TAKUKURU Dodoma yaja na Kampeni Maalum ya Ulipo Twaja

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imeanzisha Kampeni Maalum ya Uelimishaji ya Ulipo Twaja ambayo uwafuata wananchi waliopo kwenye mikusanyiko na kuwaelimisha masuala ya ubadhirifu na rushwa.

Kupitia kampeni hiyo hadi sasa wananchi 45,000 wameelimishwa kwenye mikusanyiko 88 ndani ya Mkoa wa Dodoma. 

Mkoa wa Dodoma unakadiriwa kuwa na wakazi 2,729,153 na kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 asilimia 52.2 ya watanzania ni wale wa rika la miaka 15 hadi 64, hivyo katika kampeni hiyo ya ULIPO TWAJA Takukuru Mkoa wa Dodoma imekusudia kuwafikia angalau asilimia 10 ya wananchi wa rika hilo ambao ni takribani wakazi 142,461.
Hayo yamesemwa leo Machi 2, 2022 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo wakati akizungumzia kampeni hiyo jijini hapa.

Amesema, uelimishaji huo ulioanza Januari 18, mwaka huu unalenga kuwafikia wananchi ambao wapo kwenye mikusanyiko mbalimbali.

Mkuu huyo amesema, Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuzuia na kupambana na ubadhirifu wa mali za umma badala ya kusubiri hadi zifujwe ndipo uchunguzi ufanyike.

Ameeleza kuwa wao kama taasisi ya kuzuia na kupamabana na rushwa wameona uelimishaji huo ni sahihi, kwani utawafikia wananchi wanaotumia muda mwingi katika shughuli za kujipatia riziki zao sokoni,vituo vya bajaji na bodaboda.

Sambamba na vijiwe vya kahawa au wale ambao wanaenda kupata huduma kama mikusanyiko ya wanufaika wa TASAF, siku za lishe kwenye vituo vya afya, siku za kliniki au chanjo,stendi za daladala na mabasi.

“Lengo la kampeni hii ni kuwafikia wananchi ambao kulingana na aina ya kazi au biashara wanazofanya sio rahisi kuwapata kwenye mikutano ya hadhara au mikutano mingine rasmi kama ya vijiji na mitaa inafahamika wazi wengine uendeshaji wa maisha yao hutegemea uwepo wao katika maeneo hayo ya mikusanyiko hivyo sio rahisi kuondoka na kuacha shughuli zao ili wahudhurie mikutano ya hadhara,”amesema Kibwengo. 

Pia amesema, iwapo mkusanyiko husika utakuwepo saa 12 asubuhi basi ULIPO TWAJA itawafuata na kuwaelimisha hata kama mkusanyiko huo utakuwa mchana au jioni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news