RAMADHAN KISSIMBA NA EVA VALERIAN-WFM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameiahidi Taasisi ya Africa50 kuwa Serikali imepokea maombi ya kuitaka Tanzania kujiunga na taasisi hiyo na mapendekezo hayo yatafanyiwa kazi ndani ya Wizara na Serikali na baadae kuyafikisha maombi hayo kwenye mamlaka ya juu kwa ajili ya kufanya maamuzi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akiongea na ujumbe wa Taasisi ya Africa50 (hawamo pichani), kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru na kushoto kwake ni Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Bw.Melckzedeck Mbise.
Mhe. Dkt. Nchemba ameyasema hayo jijini Dodoma alipokutana na ujumbe wa Taasisi ya Africa50 ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo Bw. Alain Ebobisse’, ambapo aliwapongeza kwa miradi wanayotekeleza ambayo kwa Tanzania ni miradi ya kipaumbele.
“Tumefurahishwa na miradi mnayotekeleza ya sekta za uzalishaji zikiwemo kilimo, nishati, mifugo na uvuvi ambayo na kwetu sisi, Serikali na nchi kwa ujumla ni miradi ya kipaumbele ambayo inayosimamiwa kikamilifu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan,"amesema Mhe. Nchemba. Afisa Mtendaji Mkuu Taasisi ya Africa50, Bw. Alain Ebobisse’ (kulia), akieleza dhamira ya kutaka ushirikiano na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kulia kwake ni Afisa Mkuu wa Uendeshaji, Bi. Tshepidi Moremong.
Mhe. Nchemba aliongeza kuwa dira ya Serikali ni kuweka nguvu kubwa kwenye sekta za uzalishaji ambazo zinachochea ukuaji wa sekta nyingine mfano uzalishaji wa nishati ya umeme na gesi, ambapo uzalishaji wa bidhaa hiyo unapaswa kupewa kipaumbele na kufanyiwa uchambuzi ili kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Taasisi ya Africa50 katika kuendeleza sekta hiyo kupitia njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Alain Ebobisse’ alisema kuwa dhamira yao kubwa ni kushirikiana na Tanzania na kuwa ipo tayari kuisaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa ile inayotekelezwa kupitia ubia kati ya serikali na sekta binafsi. Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Africa50 Bw. Alain Ebobisse’, mara baada ya majadiliano yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Pia Bw. Ebobisse’ alitumia fursa hiyo kuiomba Tanzania kujiunga na Taasisi hiyo ambayo ilianzishwa kwa lengo la kusaidia, kufadhili na kuhamasisha sekta ya Umma na binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. \ Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru kulia wakifurahia jambo na Mkurugenzi wa Uwekezaji kutoka Taasisi ya Africa50 Bw. Kaniaru Wacieni mara baada ya kumalizika kwa majadiliano ya Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango na ujumbe kutoka Taasisi ya Africa50.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).
Mhe. Mwigulu alimuhakishishia Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Africa50 kuwa Serikali itakaa na kuchambua baadhi ya miradi ambayo inaweza kukidhi vigezo ili Serikali iweze kushirikiana na Taasisi hiyo kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi ili kuweza kuwafungulia fursa vijana wa Tanzania ambao ndio wengi kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo jambo litakasaidia kukuza ajira kwa vijana na kuongeza kipato kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja.