NA MWANDISHI WETU
WIZARA ya Afya imepokea jumla ya dozi milioni 1 za chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinovac kutoka nchini Uturuki.
WIZARA ya Afya imepokea jumla ya dozi milioni 1 za chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinovac kutoka nchini Uturuki.

Waziri Ummy amesema kuwa, jumla ya dozi milioni nne za chanjo aina ya Sinovac zinatarajiwa kupokelewa kutoka nchini uturuki kwa awamu nne huku zikitarajiwa kuchanja watu milioni mbili.
"Tunaishukuru Serikali ya Uturuki kwa kutupatia ufadhili wa chanjo aina ya Sinovac, jumla ya dozi 1,000,000 kati ya 4,000,000 zinazotarajiwa kupokelewa kwa awamu nne. Chanjo hizi zinatarajiwa kuchanja watu 2,000,000,"amesema Waziri Ummy.

Waziri ummy amesema kuwa, hadi sasa jumla ya chanjo zilizopokelewa nchini ni dozi 10,845,774 zikijumuisha aina ya Sinopharm, Janssen, Moderna,Pfizer na Sinovac ambazo zinatosha kuchanja watu 6,381,327.
Amesema kuwa, hadi kufikia Machi 21, 2022 zaidi ya watu milioni 3 wamepata chanjo kamili kati ya zaidi ya watu milioni 30 wenye umri wa kati ya miaka 18 na kuendelea.
"Watu milioni 3,016,551 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30,740,928 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, hii ni sawa na asilimia 9.8," amefafanua Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka 2022, Serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya Watanzania kuanzia umri wa miaka 18.
"Niendelee, kuwasihi Wananchi, wajitokeze kwa wingi kwenda kupata chanjo na waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya UVIKO-19," amesisitiza Waziri Ummy

Aidha, ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuhimizwa kwenda kwenye vituo vya huduma za afya ili wakapate elimu kuhusu umuhimu wa chanjo na kisha kuchanja.