NA FRESHA KINASA
WAKALA wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mara umesaini mkataba na Kampuni ya Jonta Investment Company Limited ya Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili likiwemo daraja la Mto Mori na Mto Wamaya yaliyopo Kijiji cha Wamaya Kata ya Kirogo wilayani Rorya Mkoa wa Mara.
Ujenzi ambao una thamani ya shilingi Bilioni 1.4 ambapo ujenzi huo utafanyika kwa kipindi cha miezi nane.
Zoezi hilo limefanyika Machi 4, 2022 eneo la Mto Mori likishuhudiwa na wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Jumaa Chikoka ambapo akizungumzia hatua hiyo, Chikoka amesema ujenzi wa madaraja hayo mawili unakwenda kutatua changamoto za kiusalama ambapo awali wananchi walipata usumbufu wa kuvuka wakiwa na mifugo yao na wakati mwingine kupoteza maisha yao na pia litafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Ameongeza kuwa, madaraja hayo yatakuwa na umuhimu mkubwa sana kwani pia yanaendana sambamba na ujenzi wa Barabara ya Nyamaguku ambayo ni kichocheo kikubwa cha shughuli za maendeleo ya kiuchumi na pia yatawezesha kuziunganisha tarafa mbili Nyacha na Luimbo.
"Ni matumaini kwamba wananchi sasa mnakwenda kuondoka na hadha ambayo imekuwa ikiwakumba kwa muda mrefu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Hassan ni sikivu sana kwa wananchi wake, hivi majuzi nilifika Mto Mori na kukuta kijana amepoteza maisha na ng'ombe wake niliumia sana kwa tukio hilo.
"Tuendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais ameongeza fedha upande wa TARURA kutoka shilingi milioni 690 huko nyuma na sasa tumepata shilingi bilioni 3.4 upande wa ardhi tumepata bilioni moja ya upimaji ardhi, kupanga na kumilikisha. Lazima tumpongeze sana Rais kwa kazi kubwa na njema ambayo wana Rorya ametufanyia," amesema Mheshimiwa Chikoka.
Pia, Mheshimiwa Chikoka amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuwapa fursa wananchi wa maeneo hayo kusudi waweze kufanya kazi zinazowahusu katika mradi huo ili wajipatie kipato na pia akawahimiza kumpa ushirikiano Mkandarasi na wawe walinzi wa mradi. Huku TAKUKURU akiitaka kuhakikisha inadhibiti rushwa mradi huo ufanyike kwa kiwango stahiki.
Aidha, Chikoka ametoa wito kwa watu waliokusanya na kula fedha mbichi za halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuzirudisha haraka. Huku akilitaka Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji watu ambao wamehusika na ubadhirifu huo na kwamba, hana mchezo na watu wanaofuja hela za serikali kwa masilahi yao binafsi.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara, Mhandisi Boniface William amesema kuwa daraja hilo litajengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 1.4 na Mkandarasi wa Kampuni ya Jonta Investment Co.Limited kutoka mkoani Shinyanga na kwamba ujenzi utafanyika kwa kipindi cha miezi nane.
"Daraja la Mto Mori litajengwa kwa kusimika nguzo mita 10 kina kwenda chini, upana wake utakuwa mita saba na urefu wa mita 16 na pia tutajenga barabara za maingilio mita 100 kila upande. Pia tunajenga daraja la Wamaya kwa kuweka maboksi mawili urefu mita tano kwa tatu yatakuwa madaraja ya kipekee upande wa TARURA Mkoa wa Mara,"amesema.
Ores Simba Nelson ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambapo amemhakikishi mkuu wa wilaya hiyo kuwa, wananchi watalinda na kutunza mradi huo wakati wa ujenzi na baada ya kukamikika kusudi uendelee kuwanufaisha wananchi hao.
Neema Pius ni mkazi wa Kijiji cha Wamaya ambapo ameieleza DIRAAKINI BLOG kuwa, ujenzi wa daraja hilo utakuwa mwarobaini kwa wananchi kwani nyakati za mvua walipata hadha kubwa ya kuvuka na kuhatarisha usalama wao.
"Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kujenga daraja hili, Mungu amzidishie afya njema na baraka, kwani tulipata shida sana kuvuka, lakini kwa hatua hii njema wananchi tutalitumia kufanya kazi za maendeleo, tunaomba Mkandarasi afanye kazi kama ambavyo ameahidi,"amesema Ester Olio.