Ufaransa yaiwezesha Tanzania vifaa tiba kusaidia mapambano dhidi ya UVIKO-19

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI ya Tanzania leo imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka Serikali ya Ufaransa, kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Balozi Liberata Mulamula, ameishukuru Serikali ya Ufaransa kwa Msaada huo na kusema vitasaidia katika mapambano dhidi ya Uviko -19.

Amesema kwamba, msaada huo ni ishara ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Ufaransa, huku akibainisha kwamba Ufaransa imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo katika nyanja mbalimbali mathalani, elimu, miundombinu, nishati na afya.
Naye, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha uhusiano baina ya nchi ya Tanzania na nchi nyingine jambo linaloleta fursa za kimaendeleo nchini katika Sekta mbalimbali, hususan Sekta ya afya.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe.Nabil Hajlaoui amesema Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, kwani nchi hizi mbili zimekua na mahusiano mazuri ya muda mrefu.
Sambamba na hilo Mhe. Balozi Mulamula amepokea msaada wa dawa za albendazole zenye thamani ya shilingi Milioni 550 ikiwa ni ongezeko la dawa zenye thamani ya shilingi Milioni 340 zilizotolewa mwezi Februari, 2022.

Aidha, Mhe. Balozi Mulamula amewashukuru Shirika la World Vision Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya ili wananchi wapate huduma bora.
Akitoa msaada huo, Mkurugenzi wa Shirika la World Vision Tanzania Dkt. Diana Mndeme amepongeza Jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya na kuweka wazi kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za afya, hasa afya za watoto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news