Uholanzi yaahidi kuiunga mkono Zanzibar katika nyanja mbalimbali

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba utayari wa Uholanzi kuunga mkono mikakati pamoja na Sera ya uchumi wa Buluu kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliyowekwa.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo Machi 10,2022 Ikulu jijini Zanzibar katika mazunguzo kati yake na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe de Boer.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya Uholanzi kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha inaimarisha sekta zake za maendeleo ukiwemo uchumi wa ambapo nchi hiyo tayari imepiga hatua katika miongoni mwa sekta hizo.

Rais Dkt. Mwinyi alimueleza Balozi Wiebe de Boer namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoweka mikakati yake katika kuimarisha na kuuendeleza uchumi wa Buluu huku akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Uholanzi kuja kuwekeza Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alimuahidi Balozi Wiebe de Boer kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji watakaoamua kuja kuekeza Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alipongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Uholanzi na kusisitiza haja ya kuongeza ushirikiano huo hasa katika sekta mbalimbali za maendeleo ukiwemo Uchumi wa Buluu.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alimueleza Balozi huyo namna mikakati ilivyowekwa katika kuimarisha sekta nyingine za uchumi ikiwemo kilimo cha mwani na juhudi zinazochukuliwa katika kukiimarisha pamoja na sekta ya uvuvi ambapo Zanzibar inataka iondokane na uvuvi unaofanyika hivi sasa kutokana na kutokuwa na tija wala kipato kwa wavuvi pamoja na Taifa kwa ujumla.

Nae Balozi wa Uholazi nchini Tanzania Wiebe de Boer alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba Uholanzi imekuwa na uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar tokea miaka ya sitini na kusisitiza haja ya kuimarishwa.

Balozi Wiebe de Boer alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba Uholanzi iko tayari kuiunga mkono Zanzibar katika kutimiza kiu yake ya kuimarisha uchumi kupitia uchumi wa Buluu.

Alieleza kwamba kwa vile nchi hiyo tayari imepiga hatua kubwa katika sekta za uchumi wa Buluu hivyo itahakiksiha inaiunga mkono Zanzibar ili nayo ifike pale ilipokusudia ikiwa ni pamoja na kuzishawishi Kampuni kadhaa za nchi hiyo pamoja na wawekezaji kuja kuangalia mazingira ya uwekezaji ya Zanzibar.

Balozi huyo pia, alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua atakazozichukua katika kuhakikisha anaitangaza vyema Zanzibar kiutalii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunaandaliwa mazingira mazuri ya usafiri wa watalii kutoka nchi hiyo moja kwa moja hadi Zanzibar kupitia mashirika makubwa ya ndege ya nchi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news