NA MWANDISHI MAALUM, OR-TAMISEMI
WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa utezekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo ambapo kwa kupitia utekelezaji huo vijana na wanawake wapatao 150 wamenufaika na fursa za ajira.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Bw. Elkana Ngairo amesema kuwa uamuzi wa Serikali kutumia mafundi wadogo wadogo umeongeza wigo wa ajira kwa vijana, wengi wameweza kujiajiri lakini pia kuajiri wenzao. "Hii imesaidia kuwaongezea kipato lakini pia kupunguza muda wa kukaa vijiweni,"amesema.
Hayo yamebainishwa Machi 3, 2022 katika ziara ya Naibu Katibu Mkuu ( Afya) Dkt. Grace Magembe mkoani Morogoro kwa ajili ya kukagua ubora wa utolewaji wa huduma za afya na ukaguzi wa utelekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulika(Afya), Dkt.Grace Magembe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutumia mafundi wadogo wadogo na kuwataka vijana hao kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuhakikisha wanatumia uzoefu na weledi katika ujenzi wa miundombinu hiyo ili iwe imara na kudumu kwa muda mrefu.
Aidha amewataka kufanya kazi kwa weledi na kuwa waaminifu katika utendaji kazi wao ili kufungua fursa nyingine zaidi.
“Mheshimwa Rais amewaamini mafundi wadogo hivyo chapeni kazi, jengeni majengo yenye viwango vinavyohitajika ili majengo haya yadumu muda mrefu kwa faida ya jamii yote lakini pia unapofanya kazi vizuri ndipo unapofungua fursa zaidi,”amesema Dkt.Magembe.
Naye Magdalena Israel mkazi wa Halmashauri ya Mvomero amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma ya afya katika Hospitali ya Wilaya Mvomero kwa kuwa hatua hiyo imeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya hasa kwa wajawazito na watoto.