NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa, Machi 4, 2022 kiwango cha juu cha joto kinatarajiwa kuwa nyuzi 34°C katika maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Utabiri wa Hali ya Hewa wa saa 24 zijazo kuanzia saa 3 usiku leo Machi 3,2022 unaletwa na mchambuzi Akili Mwangaza kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Kwa mujibu wa TMA, mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Iringa, Mbeya, Njombe, Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Aidha, mikoa ya Lindi, Morogoro, Dodoma na Singida: Inatarajiwa kuwa na Hali ya mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Wakati huo huo, visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi na vipindi vya jua.
Upepo wa Pwani
Kwa mujibu wa TMA, upepo wa Pwani unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa kwa Pwani yote kutoka Kaskazini Mashariki kwa Pwani ya Kaskazini na kutoka Kaskazini kwa Pwani ya Kusini. Aidha, hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi ambapo mabadiliko kidogo yanatarajiwa siku ya Jumamosi ya Machi 5,2022.