NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekutana na viongozi mbalimbali wa dini na kujadili masuala ya maendeleo nchini.
Majadiliano hayo yamefanyika leo Machi 2,2022 Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Bi.Zuhura Yunus miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na elimu.
Kwa pamoja viongozi hao wamependekeza kuwepo mjadala mpana kuhusu mfumo mpya utakaokidhi mahitaji ya sasa kwa maana ya kutozalisha jamii ya wahitimu walioandaliwa kuajiriwa peke yake.
Pia, kwa mujibu wa taarifa hiyo viongozi hao wameomba kutotozwa kodi ya mapato kwenye fedha ambazo zinapatikana kama misaada ya hiari ya wanachama na wafadhili kwa ajili ya kuendesha huduma zisizo za kibiashara zikiwemo za wajane na yatima.
Wakati huo huo, viongozi hao wamelipa kipaumbele suala la uchafuzi wa mazingira huku wakitoa wito kwa Serikali kuhamasisha upandaji miti ya asili badala ya miti na mbegu za nje ambazo nazo zinahatarisha usalama wa afya za wananchi.
Mbali na hayo, viongozi hao wametumia mkutano wao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuomba mamlaka husika kutumia busara ili kuangalia namna ya kumaliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Hata hivyo, viongozi hao wametumia mkutano huo kumpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuimarisha uhusiano bora kwa nchi jirani na jamii ya Kimataifa zikiwemo fursa za uongozi kwa wanawake na kuulinda Muungano.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mbalimbali wa dini mara baada ya kikao chao kilichofanyika leo Machi 2, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.(PICHA NA IKULU).
Tags
Habari