Waandishi wa habari wathaminiwe, na tuwape ushirikiano-RC Hapi

NA FRESHA KINASA

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ally Hapi amezitaka taasisi za umma na viongozi wote wa Serikali mkoani humo kuwathamini waandishi wa habari wa mkoa huo kutokana na mchango wao mkubwa katika kufichua maovu, kutangaza kazi na miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali, hivyo amesisitiza wapewe ushirikiano katika uwajibikaji wao kwa manufaa ya wananchi.
Ameyasema hayo Machi 3, 2022 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) ambacho kilifanyikia Ukumbi wa Uwekezaji wa mkoa huo Mjini Musoma.

Amebainisha kwamba, waandishi wa habari mkoani humo wameendelea kufanya kazi nzuri ikiwemo kiripoti shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali na kufichua maovu, hatua ambayo inaisaidia pia Serikali kufanya ufuatiliaji na kuchukua hatua katika maeneo husika.

Amewaasa viongzozi katika maeneo mbalimbali mkoani Mara kujenga ushirikiano thabiti na waandishi wa habari, hatua ambayo pia itaimarisha uwajibikaji kwa viongozi katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
"Niwatake viongozi wote katika maeneo yenu jengeni ushirikiano na waandishi wa habari, zama hizi si za kufanya kazi gizani au kwa kujificha. Lazima watu wajue kazi zinazofanywa Mkoa wa Mara wapo watu wa Mkoa wa Mara wanaishi Mtwara na maeneo mengine, lakini wanafuatilia mkoa wao kwa karibu sana kuhusu nini kinafanyika. Waandishi wasipotangaza fedha za tozo zimefanya nini, au Serikali imefanya nini ni ngumu sana watu kufahamu,"amesema Mheshimiwa Hapi.

Hapi ameongeza kuwa, ataendelea kuwathamini, kuwapa ushirikiano na kushirikiana na waandishi wa habari katika kutangaza kazi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali mkoani humo ili fursa mbalimbali za mkoa wa zifahamike na zizidi kuchangia kuleta mapinduzi chanya ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news