Wabuni namna ya kukomesha mimba, kuongeza ufaulu shuleni

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SHULE ya Sekondari Kilimani iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imezindua ujenzi wa bweni la hosteli ya wasichana ukiwa ni mkakati wa kukabiliana na mimba za utotoni,utoro kwa wanafunzi wa kike na kuongeza ufaulu wao.

Akizindua ujenzi huo wa msingi wa bweni kisha akaendesha harambee ya ujenzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala,Ofisa Elimu Sekondari, Emmanuel Malima amesema, mradi huo umebuniwa na wananchi wenyewe sababu ya mahitaji ya watoto kupata muda wa kujifunza na kujisomea.
Pia amesema, wananchi na jamii wamejitolea nguvu zao, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri pia wamejitoa kuhakikisha watoto wa kike wanapata muda wa kujifunza na kujisomea kwenye mazingira mazuri yenye utulivu yatakayosaidia walimu kukuza taaluma na kuongeza ufaulu wa watoto.

Malima ameeleza mahitaji ya mabweni kwenye shule za sekondari ni makubwa na mkakati uliopo ni idara ya elimu na halmashauri kuhamasisha jamii na wananchi kuchangia miundombinu hiyo ili kupata matokeo chanya kwenye shule za Halmashauri ya Ilemela.

Amesema, bweni hilo likikamilika watoto watasoma vizuri zaidi tofauti wakitokea nyumbani ambapo aliendesha harambee ya ujenzi wa msingi wa bweni hilo na kuchangia shilingi milioni moja kwa niaba ya Idara ya Elimu Manispaa ya Ilemela.

Mmoja wa wadau wa shule hiyo, Mhandisi Mnandi Mnandi,alisema kauli mbiu ya Kilimani ni kutokomeza sifuri na daraja la nne,hivyo alichangia sh. 350,000 na kuahidi kununua viti vya walimu na akawataka wazazi kujitathmini na kuchangia elimu ya watoto wao.
 
Baadhi ya wanafunzi wa hosteli,Getruderose Joseph wa kidato cha nne na Nuryat Mohamed wa kidato cha kwanza,walisema kuishi hosteli ni tofauti na nyumbani,kumewaongezea ari ya kujifunza zaidi sababu ya madhari na mazingira tulivu ya kujifunzia.

Getruderose amesema, watoto wa kike kupata elimu wakitokea nyumbani ni kazi,njiani wanakumbana na changamoto nyingi,nyumbani wanafanya shughuli nyingi za kusaidia familia na kukosa fursa ya kujisomea tofauti na hosteli ambapo aliahidi kuwekeza mshahara wake kwenye ujenzi wa chuo cha marubani nchini baada ya kuhitimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news