Wanafunzi wa kike Shule ya Sekondari Macechu waomba kujengewa vyoo

>Wasema kuna uhaba wa vyoo vya wasichana, hivyo kuwatatiza wakati wa kujistiri wakiwa kwenye hedhi

NA HADIJA BAGASHA

WANAFUNZI wa kike zaidi ya 600 wa Shule ya sekondari Macechu iliyopo jijini Tanga wamelalamikia uhaba wa vyoo vya wasichana jambo ambalo limekuwa likisababisha hadha kwao wakati wanapokwenda kujistiri wanapokuwa kwenye hedhi huku baadhi yao wakikosa masomo kwa kubaki majumbani kwa kuhofia usalama wao.Wakizungumza wakati walipokuwa wakipokea taulo za kike shuleni hapo wanafunzi hao wameomba msaada wa vyoo kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

Scolastika Mtweve ni mmoja wa wanafunzi shuleni hapo anasema, kitendo cha shule yao kuwa na uhaba wa matundu ya vyoo kimekuwa kikiwaathiri pale tu wanapoingia kwenye mzunguko wa hedhi jambo ambalo limekuwa likiwaathiri kitaaluma.
Wanafunzi hao wameomba kuongezewa vifaa vya kuhifadhia taka vitakavyotumika kuhifadhia taulo za kike ambazo zitakuwa zimetumiwa na wanafunzi.

"Sisi wanafunzi hapa shuleni ni wengi hivyo kitendo cha kuwa na matundu machache ya vyoo kinatupa wakati mgumu sana sisi wanafunzi wa kike inafika wakati tunaogopa kuka shule kwa kuhofia usalama wetu,"amesema Scolastika.
Kwa upande wake Mlezi wa wasichana shuleni hapo, Shafii Mbombe amekiri kuwepo kwa uhaba wa matundu ya vyoo jambo ambalo linasababisha hadha kwa wanafunzi wawapo shuleni hapo.

Mlezi huyo ametoa wito kwa taasisi nyingine kusaidia tatizo hilo ili kuweza kuwasaidia wanafunzi kuzingatia masomo yao ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu kwa watoto wa kike.

Mwanaidi Mhina ni Makamu mkuu wa shule hiyo amesema, msaada waliopatiwa shuleni hapo umekuja kwa wakati muafaka ambao watoto hao walikuwa wakiuhitaji huku akionyesha umuhimu wa jambo hilo kwenye maendeleo ya kitaaluma.

Kwa upande wake Zahra Omari ambaye ni Afisa wa Shirika la Bima la Zanzibar kutoka makao makuu amesema kuwa, maombi ya wanafunzi hao ni ya msingi kutokana na umuhimu wa vyoo kwa maisha ya jamii.
"Inakuwa, ni vigumu sana mwanafunzi anapoingia kwenye siku zake halafu akashindwa kupata huduma hiyo akapata shida ya maji na kujisaidia kwa kweli inasikitisha mno inatakiwa mwanafunzi apate hayo yote ili awe huru kuingia darasani mimi nimepokea maombi yenu na nitawasilisha panapohusika na muda mfupi Mwenyezi Mungu ajaalie mpate mnachokitaka, "amesema Zahra.

Hassan Abdalah ni Meneja wa Shirika la Bima la Zanzibar ofisi ya Tanga amesema, wamefikia hatua ya kuamua kuwasaidia wanafunzi hao taulo za kike baada ya kubainika kwamba wengi wanashindwa kuhudhuria shuleni kwa sababu wanakosa huduma hiyo na kuathirika kitaaluma.

Hassan amesema shirika hilo kama mdau wa maendeleo litaendelea kusaidia wanafunzi pale ambapo itawezekana kama sehemu mojawapo ya sehemu ya faida wanayoipata.
Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo Halmashauri ya Jiji la Tanga itatumia kiasi cha shilingi milioni 319 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo vya walimu, wanafunzi wa kawaida na wenye ulemavu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news