Wanawake Jiji la Dodoma washauriwa kufanya kazi kwa bidii, mshikamano

NA DENNIS GONDWE

WANAWAKE katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kufanya kazi kwa bidii na mshikamano ili kuhakikisha jiji hilo linasonga mbele katika nyanja zote za maendeleo.
Wito huo ulitolewa na Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sekunda Kasese katika mahojiano maalum na Dodoma City TV ofisini kwake.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwashauri wanawake katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa na mshikamano ili kuhakikisha jiji letu linasonga mbele katika nyanja zote za maendeleo,”almesema Mratibu Kasese.

Akiongelea kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka 2022 isemayo “Kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu; tujitokeze kuhesabiwa” ameitaja kuwa ni muhimu. "Kaulimbiu hiyo ni muhimu sana kushirikisha jinsia zote katika mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla,"ameongeza.

“Wanawake ni kundi kubwa sana katika jamii na wao wakishirikishwa katika mipango ya maendeleo, wanawake wanaweza na wanafanya vizuri. Hivyo, wakijitokeza kuhesabiwa kwa sababu ni sehemu kubwa ya jamii yetu wataiwezesha serikali kufikia malengo yake,”amesema Mratibu Kasese.

Kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii amesema kuwa, unafanya vizuri.

“Mpango wa kunusuru kaya masikini unafanya vizuri na unaendelea kufanya vizuri katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuinua hali ya umaskini wa jamii. Kundi kubwa la walengwa walio katika mpango wa kunusuru kaya masikini ni wanawake.

"Katika Jiji la Dodoma tuna jumla ya wanufaika 26,289, kati ya hao 16,101 ni wanawake walio katika rika mbalimbali na 10,188 ni wanaume. Wengi wanaopokea ruzuku ni wanawake.

"Tunajua mwanamke akipokea ruzuku ni fedha inayomsaidia yeye pamoja na kaya kwa ujumla sababu anapochukua fedha hiyo haipeleki katika mambo mengine yasiyofaa mfano ulevi wa kupindukia. Fedha anayopata anaipeleka kwenye biashara ndogondogo na shughuli nyingine za uzalishaji mali ili kuongeza kipato cha kaya,” amesisitiza Mratibu Kasese.

Mratibu huyo amesema kuwa, wanawake wanufaika wa TASAF walio katika vikundi wanapata fursa ya mikopo ya wanawake ya asilimia nne kutoka mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri ya jiji hilo.

“Ni ukweli usifichika kuwa mikopo inayotolewa na halmashauri kutoka mapato ya ndani imewanufaisha wanawake wengi tu wanufaika wa TASAF,”amesema.

Amesema kuwa, wanawake hao wamekuwa wakinufaika na mafunzo ya ujasiriamali kupitia ‘community sessions’ ambazo wakufunzi mbalimbali hutoa elimu ya ujasiriamali, masuala ya lishe, ufugaji, utengenezaji sabuni na vyungu.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2022 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kizazi cha haki na usawa kwa naendeleo endelevu, tujitokeze kuhesabiwa" na ngazi ya Mkoa wa Dodoma yatafanyika wilayani Chemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news