Wanawake wafunguka kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametajwa kuwa kiongozi shupavu, jasiri, mzalendo na muwajibikaji kwa nchi yake katika kuhakikisha Taifa linazidi kusonga mbele katika nyanya mbalimbali ikiwemo kijamii na kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Machi 5, 2022 kupitia Mjadala wa Kitaifa unaoratibiwa na Watch Tanzania ukiangazia Wanawake na Uongozi kuelekea Mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.

Mjadala huo ambao umefanyika kwa njia ya Zoom umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kampuni ya Simu za Mikononi Tanzania ya Airtel.

Balozi Mongella

Mwanasiasa mkongwe hapa nchini, Balozi Getrude Mongella wakati akishiriki katika mjadala huo wa kitaifa ulioangazia wanawake na uongozi; kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani ambao umeshirikisha wazungumzaji mbalimbali wakiwemo viongozi wanawake kutoka serikalini, taasisi binafsi na mashirika ya Kimataifa amesema kuwa, tangu Rais Samia Hassan ameingia madarakani yapo mambo mengi ya kujivunia.

Pia amesema, Rais Samia ameweza kuyatekeleza yahusuyo maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii kwa Watanzania na yamezidi kulifanya taifa kupiga hatua.

Amebainisha kuwa, Rais Samia ameweza kuwaheshimisha wanawake na kuuonesha ulimwengu kuwa yeye ni kiongozi mwanamke mwenye uwezo thabiti wa kuongoza na kuliwezesha kudumu katika misingi ya umoja, amani, utu na mshikamano wa kitaifa ambao umezidi kuwaweka pamoja Watanzania wote.

Amesema, Watanzania wanaendelea kuishi kwa amani na utulivu na kwamba hawana hofu kama ambavyo baadhi yao walidhani kwamba nchi ingeyumba baada ya mtangulizi wake Hayati John Magufuli kufariki dunia na nafasi hiyo kuwa mikononi mwake, lakini ameendelea kusimamia imara na kuwajibika kikamilifu kwa maslahi mapana ya nchi.

Pia amesema kuwa, Rais Samia ameweza kuvunja mwiko kwa kuwa kiongozi mwanamke wa kwanza kuliongoza taifa, na amemudu vyema kupanua wigo wa viongozi wanawake katika taifa kwa kuwaamini na kuwapa nafasi mbalimbali, hali ambayo inaimarisha usawa katika taifa huku akiwataka wanawake kumtumia Rais Samia kama fursa ya kuzidi kufikia malengo chanya kwa manufaa kutokana na dhamira yake njema.

Aidha, Balozi Mongella amesema kuwa elimu ya TEHAMA kwa watu wazima ni muhimu ikapewa kipaumbele katika taifa, kwani itawezesha pia watu kufikia mafanikio na kuweza kunufaika na fursa mbalimbali pamoja na kila mmoja kushiriki katika juhudi za kuondoa umaskini akasisitiza mkazo uwekwe katika elimu katika kuandaa wasomi watakaozidi kuleta mapinduzi chanya ya kimaendeleo.

Balozi Dkt.Chana

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dkt.Pindi Chana maesema kuwa,kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuna mambo makubwa yamefanyika kuanzia maboresho, maendeleo na mikakati katika maeneo mengi nchini.

"Tunapozungumzia mwezi huu wa Malikia wa Nguvu. Tunapozungumzia mlingano wa majukumu, kwanza kabisa tunaona dhamira ya dhati ya Serikali iliyopo madarakani ya kuanzisha wizara maalum.Tunayo wizara inayoshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunayo wizara inayoshughuilikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto.

"Tukumbuke kwamba, zipo nchi hazina hata Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wao wana wizara zingine, lakini sisi dhamira ya mlingano wa majukumu, masuala ya jinsia, genda, wizara maalum ipo. Ina bajeti yake. Na sasa Mheshimiwa ameona badala ya kuchanganya na masuala ya afya, tutakuwa na waziri wa afya na tutakuwa na waziri wa maendeleo ya jamii.

"Hiyo peke yake inaleta dhamira ya dhati, maana yake bajeti tofauti, makatibu wakuu ambao wanashughulikia wizara hizo. Pamoja na kuwa na wizara hizi na wataalamu wake mahususi, Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho maeneo mengi,"amesema.

Amesema maboresho yameanzia katika elimu ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imejenga madarasa ya awali, msingi na sekondari. Lengo ni kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule bila kipingamizi chochote nchini.

Kwa upande wa maji, Mheshimiwa Balozi Dkt.Chana amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imekuwa mstari wa mbele kumtua mama ndoo kichwani kupitia miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa kuanzia vijijini hadi mijini.

Aidha,amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali ikiwemo kuwawekea mazingira bora ya kufanya kazi zao ili kuwainua na kuimarisha vipato vyao.

Kwa upande wa teuzi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu umewapa nafasi mbalimbali wanawake ambao wamekuwa wakionesha ufanisi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa maslahi mapana ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Balozi Kanza

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Marekani,Mheshimiwa Elsie Kanza amesema kuwa, anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuzalisha wanawake wengi kuwa viongozi ambao wanachapa kazi kwa ufanisi.

Huku akitolea mfano kuwa Taifa la Marekani licha ya kuzidi kupigania haki za wanawake bado halina Rais mwanamke kama ilivyo kwa Tanzania.

"Licha ya Marekani kuwa nchi ya kwanza kabisa kupigania haki za wanawake na usawa wa kijinsia duniani, haijawahi kuwa na Rais mwanamke, hivyo pia Wamarekani wanalakujifunza kutokea kwetu (Tanzania) hasa kwenye suala la uongozi na usawa wa kijinsia,"amesema Balozi Mheshimiwa Kanza.

Ameongeza kuwa, wapo wanawake mbalimbali duniani ambao mchango wao unazidi kutambuliwa na kuthaminiwa katika masuala ya uvumbuzi wa kisayansi na wameweza kufanya vyema katika uvumbuzi wa dawa ya tiba za malaria.

Pia akatolea mfano makampuni makubwa 500 nchini Marekani kati ya hayo 41 yanaongozwa na wanawake, hivyo wanawake wazidi kuaminiwa na kupewa nafasi zaidi.

UN Women

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) nchini Tanzania, Hodan Addou amesema, Rais Samia anania thabiti na ya dhati katika kuimarisha usawa kwani ameweza kuwaamini wanawake wengi katika nafasi serikalini.

Sambamba na ngazi kubwa wakiwemo mawaziri na wanafanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa, na pia yeye ameendelea kuwa alama nzuri katika uongozi ndani ya Tanzania, Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.

"Nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake kama Rais, najua sio kitu kidogo ila imani yangu ataendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania duniani kote.

"Ukiangalia katika takwimu za Dunia utagundua kwamba ni asilimia 26 za nafasi za juu za uongozi zinashikiliwa na wanawake na ni nchi 10 duniani zinazoongozwa na Rais wanawake na Tanzania ni miongoni mwa hizo nchi 10 zinazoongowa na mwanamke.

"Tangua uongozi wa Awamu ya Sita kuingia madarakani kumekuwa na ongezeko la viongozi wanawake katika ngazi tofautitofauti za Serikali.

"Mfano asilimia 28 ya mawaziri ni wanawake, asilimia 36 ya wabunge Bara ni wanawake, asilimia 38 ya wabunge Zanzibara na asilimia 30 ya viongozi katika ngazi za Serikali za mitaa,"amesema Bi.Addou.

Madam Rita

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benchmark Productions, Madam Rita Paulsen anasema kuwa, Rais Samia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja amefanya mambo mengi makubwa ikiwemo kuondoa mwingiliano wa taasisi na taasisi katika kuongeza ufanisi ili kutoa huduma bora kwa wadau mbalimbali.

"Rais Samia alivyoingia madarakani na kutenganisha Wizara ya Utamaduni , Sanaa na Michezo na Ofisi ya Habari imekuwa ni jambo jema mno.

"Kwani kulikuwa na mwingiliano mkubwa wa kazi na utendaji ila leo tunajionea ofisi hizi mbili zikifanya majukumu yake vizuri sana na ufanisi kuongezeka kila mwanasanaa anafurahia.

"Pia Mheshimiwa Rais amekuwa kijitia sana katika shughuli a sanaa na amekuwa mstari wa mbele kwenye hafla mbalimbali zinazohusu burudani na sanaa, kwani tumeshuhudia akipiga simu mbalimbali kwenye matamasha ya burudani na kuwapa moyo wasanii wetu,"amesema Madam Rita.

Dkt.Elieshi Mungure

Kwa upande wake Katibu wa Afrika, Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani katika Ofisi Kuu ya Geneva nchini Uswisi, Dkt.Elieshi Mungure amesema kuwa, Mungu amemejalia Rais Samia kipawa kikubwa cha uongozi.

"Pia Mungu amemjalia kipawa cha upendo, utu, kujali na unyenyekevu kwa ujumla mama anafikika.Rais wetu amejitahidi sana kuhakikisha anaboresha sera kuleta unafuu hasa kwa mtoto wa kike, mfano tumeshuhudia watoto waliokuwa na ujauzito wanarudi shule, ujenzi wa shule maalum na sayansi kwa watoto wa kike, sera za afya na maradhi na nyinginezo,"amesema.

Sheba Kusaga

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Maendeleo ya Biashara wa Clouds Media Group, Bi. Sheba Kusaga anasema kuwa, ushirikiano anaoutoa Mheshimiwa Rais Samia kwenye sekta binafsi hata kwenye kuweka unafuu kwenye vigezo na masharti katika uwekezaji ni jambo la faraja.

"Kiukweli unaona utofauti kwa uchumi pamoja na kwamba alikuta umekaa vibaya sana, tunamshukuru ameweza kutoa nafasi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambao kwa kiasi kikubwa wanadumisha chapa nyingi ambazo zina maendeleo endelevu.Sisi Clouds tutaendelea kufungua fursa kwa kuhabarisha, fursa ambazo zina mondo wa Serikali, tukiwa tunaburudisha, lakini pia tukiwa na mchango katika tasnia ya muziki kwa kutengeneza ajira ambazo nyingine ni rasmi na nyingine si rasmi,"amesema Bi.Kusaga.

Barbara Gonzalez

Wakati huo huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez amesema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wauongozi wa Rais Samia amejifunza mambo matatu kwake.

"Kuna vitu vitatu mimi kama Afisa Mtendaji Mkuu nimejifunza kwenye uongozi wa Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, kwanza ni uvumilivu na utulivu.

"Pili ni namna bora ya kudeal na pressure ndani ya taasisi na nje ya taasisi. Jambo la tatu ni ujasiri na namna bora ya kuongoza taasisi kubwa ambayo inagusa maisha ya watu, pamoja na watu zaidi ya milioni 60 ambao wanaishi hapa Tanzania,"amesema Gonzalez.

Amesema, kupitia mambo hayo yamemuwezesha Rais Samia kushughulikia masuala mbalimbali yenye maslahi kwa taifa pamoja na ujasiri mkubwa ambao umeendelea kuliweka taifa katika hali ya utulivu na usalama.

Pia amesema, aina ya uongozi wa Rais Samia imewaonesha mfano mzuri juu ya namna ya kuongoza na kuondokana na mfumo dume ambao ulikuwepo.

"Mama Samia anavyodeal na hizi changamoto ananionesha namna ya kudeal na umma, namna ya kubadilisha mitazamo siku hadi siku, leo unaweza kuama ukakuta mjadala fulani kwenye vyombo vya habari na mitandao na mchana ukabadilika. Hivyo kwa niaba ya Simba SC na wadau wote kwenye mpira tunampongeza sana Mama Samia kwa uongozi wake wa mwaka mmoja na pia kama mwanamke kwenye nafasi ya kuongoza taasisi na pia ninampongeza kwa kunionesha mfumo imara wa uongozi,"amesema.

DC Jokate

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Jokate Mwegelo amesema kuwa, Rais Samia ni kiongozi wa kipekee na ni mwanamke aliyejipambanua kwani ameweza kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoachwa na mtangulizi wake Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Magufuli.

Amesema,pia ameanzisha miradi yake ambayo ni alama kubwa kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo kwa kiwango kikubwa vimewezesha wanafunzi waliofaulu wote kupata nafasi ya kusoma bila usumbufu.

"Tumeona Mheshimiwa Rais Samia amekuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tangu ameshika nafasi hii, kuna mambo mengi ameweza kuyafanya ikiwemo kimaendeleo na amekuwa akifanya kazi bila kuchoka.

"Pia amefanya yale ambayo yaliachwa na Serikali iliyopita ameanzisha yeye mwenyewe legacy yake, ambacho ndiyo cha muhimu, kwa namna ambavyo anatekeleza majukumu yake kama Mheshimiwa Rais, hiyo inatupa sisi kujua kwamba wanawake hatuna jambo ambalo hatuwezi kulifanya. Tumeumbwa na uwezo, akili na ufanisi na Rais ameumbwa na mfano hai,"amesema Mheshimiwa Jokate.

Amesema kuwa, uongozi wa Rais Samia umekuwa ni hamasa tosha. "Na mimi nimwambie kuelekea 2025 wanawake wengi, mimi nina imani watajitokeza kugombea, kwani wana imani Mheshimiwa Rais atawaangalia wanawake kwa jicho la tofauti,"amesema Mheshimiwa Jokate.

Flaviana Matata

Naye Flaviana Matata ambaye ni Mkurugenzi wa Lavy Company na Wakfu wa Flaviana Matata (Flaviana Matata Foundation) anasema kuwa, alichojifunza kwa Rais Samia ni moyo wa huruma, uongozi shirikishi na utu.

"Kupitia uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani nimeweza kujifunza vitu vikuu vitatu ambavyo ni uongozi shirikishi, utu, utulivu na ujasiri.Kwenye uongozi shirikishi tumemuona Rais Samia akishirikisha makun di mbalimbali na yeynye rika tofauti tfauti katika kufanikisha malengo yake ambayo amejiwekea kufikia ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

Ameongeza kuwa, katika utu na uvulivu kila mmoja ameona Rais Samia aliingia madarakani katika njia ambayo hatukuwahi kuzoea ila ipo kwenye katiba.

"Rais amekuwa na utulivu mkubwa sana, maana wengi wetu hatukujua kama nchi itafika hapa tulipo, hivyo ni pongezi nyingi sana kwake,"amesema Bi.Matata.

Angellah Kairuki

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Kizazi cha Usawa wa Kijinsia, Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema kuwa,ana imani kubwa na uongozi wa Rais Samia kwani, tangu huku nyuma alionesha jitihada kubwa ambazo zilileta matokeo makubwa kwa Taifa.

Amesema kuwa, Rais Samia ameendelea kuwagusa wanawake katika kuhakikisha kwamba uchumi wao unazidi kuimarika ikiwemo kuhakikisha wananufaika na mikopo mbalimbali, kushiriki katika masuala mbalimbali ikiwemo haki na usawa kiuchumi kwa wanawake.

Pia kushiriki katika mabadiliko ya tabia nchi, na pia amezidi kuhakikisha huduma za upatikanaji wa maji kwa wepesi katika maeneo yao pamoja na huduma za afya ili kusudi kuchochea maendeleo yao na taifa kiujumla.

Amesema, kuanzia mwaka 2016 Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweza kuteuliwa katika Jopo la Watu Mashuhuri Duniani kwa ajili ya kuangalia suala la haki za kiuchumi kwa wanawake.

Sambamba na uwezeshaji na aliwawakilisha vizuri wakati huo na jukumu hilo lilikuwa na mafanikio makubwa.

"Mwaka 2020 tumeona kwamba Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la UN Women kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa na Mexico waliweza kuandaa Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa. Hii ni kutokana na kazi nzuri aliyoweza kuifanya Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) wakati huo kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ndiyo ikaweza kuzaa jukwaa hili la kizazi chenye usawa,"amesema.

Pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwani anasema, Serikali ilitambua changamoto kubwa ambayo inawakabili wanawake hususani kuhusu upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kufanyia biashara.

"Serikali kwenye eneo hili wameona ni kwa namna gani benki zitapunguza riba na sasa kupitia kilimo, watu wameanza kunufaika na mikopo yenye riba nafuu chini ya asilimia tisa. Ni imani yangu kuwa, benki nyingine zitaendelea kupunguza,"amesema.

Pia Mheshimiwa Kairuki amesema kuwa, kupitia uongozi wa Rais Samia ana matumaini makubwa kuwa,wanawake wataendelea kuneemeka zaidi kupitia uwezeshwaji kiuchumi.

"Ninaamini itakapofika mwaka 2025 kupitia mpango wa miaka wa maendeleo, kupitia Rais Samia tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana,"amesema.

CEO Round Table

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa CEO Round Table Tanzania (CEORT), Santina Majengo Benson amesema kuwa, hatua ya Rais Samia kuimarisha Diplomasia ya Uchumi ni ishara njema kwa Tanzania kuwa na uwekezaji mkubwa ambao utaleta matokeo makubwa.

Amesema, Diplomasia ya Uchumi ni muhimu kwenye suiala la uchumi kwa Taifa lolote duniani ikiwemo Tanzania. "Tumeshuhudia dhamira njema ya Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) ya kuboresha mazingira haya ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuibdanr Tanzania. Alitumia muda wake kuhakikisha anaonesha vivutio vya utalii.

"Rais ametembelea nchi mbalimbali kuanzia Afrika, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na hivi juzi Dubai, hizi jitihada zinatoa ishara kali kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwamba, Tanzania ni nchi yenye kuvutia wawekezaji,"amesema.

Bi.Santina anasema kuwa, CEO Round Table Tanzania wanaunga mkono juhudi hizo za Mheshimiwa Rais Samia kwani wanatambua umuhimu wa kuendesha biashara kwa namna yenye kuleta matokeo chanya katika jamii.

Pia amebainisha kuwa, CEO Round Table inawakilisha wakurugenzi kutoka kampuni zaidi ya 60 nchini Tanzania na wapo katika sekta mbalimbali kwa lengo la kudumisha ushirikiano wa karibu kati ya sekta za umma na binafsi.

"Lengo kubwa ni kuongeza kasi ya upanuzi na ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa njia endelevu.Wanachama wa CEO Round Table wanachangia uchumi wa Tanzania kupitia ushuru, ajira, uhamishaji wa teknolojia na kukuza ujuzi.

" Na hili kuhakikisha tunafanikiwa kwenye malengo tuliyopanga, sisi tunaongozwa na kanuni za Ethical Leadership na tumetambua sehemu nne muhimu ikiwemo nguzo ya maadili, ushiriki, sera na uendelevu,"amesema Bi. Santina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news