OUAGADOUGOU-Zaidi ya watu 10 wanahofiwa kufariki kutokana na shambulio lililotekelezwa na watu wenye silaha kwenye mgodi mmoja wa dhahabu uliopo Kaskazini mwa Burkina Faso.
Tukio hilo ambalo limetekelezwa Machi 13, 2022 huko Baliata Mkoa wa Sahel lilitokea siku mbili baada ya shambulizi jingine kama hilo lililotokea eneo la karibu.
Picha na AFP.
Burkina Faso, ambayo ina maana ya ardhi ya watu waaminifu, ina akiba kubwa ya dhahabu, lakini nchi hiyo inakabiliwa na wasiwasi wa ndani na nje juu ya hali ya uchumi wake na haki za binadamu huku rasilimali madini zikionekana kuwanufaisha wachache.
Koloni hilo la zamani la Ufaransa, lilipata uhuru kama Upper Volta mwaka 1960. Taifa la Burkina Faso ambalo lina kiwango kikubwa cha uzalishaji wa madini ya dhahabu barani Afrika, linatajwa kushika nafasi ya tano katika uzalisha wa madini hayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, tukio hilo lilitekelezwa na watu wasiojulikana wenye silaha ambao walifanya shambulio hilo kwenye mgodi wa madini ya dhahabu katika eneo hilo.
Machi 10,2022 watu 14 waliuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia mgodi wa dhahabu katika mji wa Seytenga wa jimbo la Séno lililopo Kaskazini mwa nchi hiyo.
Pia mwezi Februari kulitokea mlipuko mkubwa karibu na mgodi wa dhahabu uliopo Kusini Magharibi mwa Burkina Faso na kuua watu 60 na kujeruhi wengine zaidi ya 100
Ni mlipuko ambao ulitokea katika ghala la kemikali zinazotumiwa kusafishia madini ya dhahabu.