NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WATANZANIA wametakiwa kuenzi ujasiri uliooneshwa na Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dk. John Magufuli wa kuijenga Tanzania na kuingia uchumi wa kati kabla ya muda uliokuwa umepangwa kufika.
Hayo yamebainishwa leo Machi 25, 2022 jijini Mwanza na wazungumzaji mbalimbali katika kongamano la kumkumbuka Rais Dk. Magufuli baada ya mwaka mmoja wa kifo chake.
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden,Dkt.Wilbroad Slaa alisema kutokana na nchi kufikia kipindi, ambacho haki na dhuluma ziliongezeka nchini, alihitajika kiongozi ambaye ni jasiri kutokomeza maovu kwa Watanzania.
"Ilifikia kipindi mwananchi aliyeko kijijini alitozwa mifugo yake kwa nguvu na viongozi waliotumia madaraka yao vibaya, akikataa anabambikiziwa kesi ya mauaji na kutupwa gerezani, hivyo hali hiyo ilihitaji Rais jasiri kuleta mabadiliko,"amesema Dkt.Slaa.
Amesema, mataifa ya Afrika hayana budi kutafakari aina ya demokrasia ya kufuata kulingana na hali halisi iliyo nayo, hivyo kuepuka kufanya lawama kwa viongozi walioko madrakani.
Mbunge mstaafu wa Maswa, John Shibuda amesema kuwa, kuliibuka kwa walaji ambao walipitia migongo ya watu, hata hivyo kutokana na ujasiri wa Dkt.Magufuli aliwezesha kuwepo usawa baina ya makundi ya watu masikini na matajiri.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Prof. Costa Mahalu amesema kutokana na mchango mkubwa uliofanywa na Magufuli , Tanzania imeanza kuchukua hatua za kimaendeleo kwa kasi kubwa.
Amesema, kama taasisi ya elimu ya juu wataendelea kutoa machapisho ya yale mema yaliyofanywa na viongozi wa taifa hili, ili kutumika katika maendeleo ya taifa na kwa taaluma.
Mhadhiri wa Uchumi Chuo cha SAUT, Dkt.Anne Gongwe amesema kuanza kutekeleza miradi mikubwa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (SGR), madaraja makubwa ni ushahidi wa dhamira njema iliyooneshwa ya kuwatumikia Watanzania.
Pia amesema, kuwepo kwa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi ama daraja la JPM pamoja na kuwepo utaratibu wa Elimu Bure kwa Watanzania ni baadhi ya ushuhuda wa utumishi imara wa hayati Dkt. Magufuli.