NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dkt.Pindi Chana amesema, wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano muda wote kwa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kwani baraza hilo limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa uchumi nchini.
Amesema, baraza hilo ni kati ya majukwaa ya majadiliano na ushauri nchini ambayo yamekuwa na matokeo chanya kwa kuziunganisha sekta ya umma na binafsi.
"Suala la kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini ni hatua njema sana, kwani yanachangia kwa kiwango kikubwa uwekezaji kupitia rasilimali zetu za ndani, hivyo kufungua fursa za kukuza uchumi na ajira.
"Ninyi mnaupiga mwingi sana, hongereni kwa hilo. Niwaahidi tu kwamba, wizara itaendelea kushirikiana nanyi wakati wote ili kuendelea kutoa nafasi ya kujadiliana namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kuanzia ngazi za chini ikiwemo wilaya, mikoa hadi Taifa.
"Mmekuwa na mchango mkubwa sana wa kutengeneza mazingira bora ya kufanyia biashara na uwekezaji,kuibua fursa za uwekezaji na kuzinadi fursa hizo kupitia makongano mbalimbali ndani na nje ya nchi;
Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana ameyasema hayo Machi 18, 2022 wakati alipofanya ziara katika za Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza, kusikiliza changamoto wanazokabiliana nazo ili kuona namna Serikali itakavyozipatia ufumbuzi kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa baraza hilo.
Pia ametoa rai kwa mabaraza ya wilaya na mikoa kuhakikisha yanashiriki kikamilifu katika mikutano hiyo kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa ya Kalenda ya Mikutano ya Majadiliano.
"Mabaraza ya mikoa na wilaya yanapaswa kukutana na kukaa kwa mujibu wa ratiba, haya majadiliano ni muhimu mno katika kuboresha mazingira ya biashara kwenye maeneo yetu, tusisubiri hadi tusikie viongozi wa Kitaifa wanafika katika mikoa na wilaya zetu ndiyo tuanze kukimbizana,kupitia mabaraza haya Taifa litapiga hatua kubwa kiuchumi,"ameelekeza Waziri Balozi Dkt.Chana.
Dkt.Wanga
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt.Godwill Wanga amesema, baraza hilo ni daraja muhimu baina ya sekta ya umma na binafsi nchini.
Amesema, baraza hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan linaundwa na wajumbe mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi nchini.
"Hiki ni chombo muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu katika nyanja za biashara na uwekezaji. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji sana nchini, hivyo tuna jukumu la kuwaunganisha wadau wote ili waweze kushiriki katika fursa hizo,"amesema.
Pia amesema, Tanzania ina fursa nyingi za biashara na uwekezaji ikiwemo kwenye sekta za utalii, miundombinu, kilimo na biashara na nyinginezo ambazo ni njia za haraka za kukuza uchumi.
Amesema, wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha baraza hilo ambalo lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na.1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na.39 la Septemba 28, 2001 linazidi kuwa daraja muhimu baina ya sekta ya umma na binafsi katika kujenga uchumi imara na endelevu nchini.
Dkt.Wanga amesema, jambo ambalo wanajivunia zaidi wao kama baraza ni pamoja na kufanikisha kujenga kuaminiana baina ya sekta binafsi na umma jambo ambalo linatoa faraja zaidi ya kuwezesha umoja huo kuwa nguzo muhimu ya kustawisha uchumi na kuharakisha maendeleo nchini.
"Tutaendelea kuratibu na kusimamia ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za maendeleo nchini, tunaamini kuwa, majadiliano na maazimio ni nguzo muhimu katika maendeleo,"amesema.
Waziri
Aidha, Waziri Balozi Dkt.Chama amesema kuwa, changamoto na maoni ambayo wameyawasilisha watayafanyia kazi hatua kwa hatua, huku akitoa rai kwa watumishi wa baraza hilo kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi ili kufanikisha mipango na dhamira njema ya Serikali ya kulianzisha baraza hilo kwa manufaa ya jamii na Taifa.