NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dkt.Pindi Chana maesema kuwa,kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuna mambo makubwa yamefanyika kuanzia maboresho, maendeleo na mikakati katika maeneo mengi nchini.
Ameyasema hayo leo Machi 5, 2022 kupitia Mjadala wa Kitaifa unaoratibiwa na Watch Tanzania ukiangazia Wanawake na Uongozi kuelekea Mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.
Mjadala huo ambao unafanyika kwa njia ya Zoom umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kampuni ya Simu za Mikononi Tanzania ya Airtel.
"Tunapozungumzia mwezi huu wa Malikia wa Nguvu. Tunapozungumzia mlingano wa majukumu, kwanza kabisa tunaona dhamira ya dhati ya Serikali iliyopo madarakani ya kuanzisha wizara maalum.Tunayo wizara inayoshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunayo wizara inayoshughuilikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto.
"Tukumbuke kwamba, zipo nchi hazina hata Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wao wana wizara zingine, lakini sisi dhamira ya mlingano wa majukumu, masuala ya jinsia, genda, wizara maalum ipo. Ina bajeti yake. Na sasa Mheshimiwa ameona badala ya kuchanganya na masuala ya afya, tutakuwa na waziri wa afya na tutakuwa na waziri wa maendeleo ya jamii.
"Hiyo peke yake inaleta dhamira ya dhati, maana yake bajeti tofauti, makatibu wakuu ambao wanashughulikia wizara hizo. Pamoja na kuwa na wizara hizi na wataalamu wake mahususi, Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho maeneo mengi,"amesema.
Amesema maboresho yameanzia katika elimu ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imejenga madarasa ya awali, msingi na sekondari. Lengo ni kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule bila kipingamizi chochote nchini.
Kwa upande wa maji, Mheshimiwa Balozi Dkt.Chana amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imekuwa mstari wa mbele kumtua mama ndoo kichwani kupitia miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa kuanzia vijijini hadi mijini.
Aidha,amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele kuwajengea wananchi uwezo wa kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali ikiwemo kuwawekea mazingira bora ya kufanya kazi zao ili kuwainua na kuimarisha vipato vyao.
Kwa upande wa teuzi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu umewapa nafasi mbalimbali wanawake ambao wamekuwa wakionesha ufanisi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa maslahi mapana ya Taifa na jamii kwa ujumla.