NA ANGELA MSIMBIRA,OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kuwachukulia hatua za kiutumishi wakuu wote wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi kwenye ujenzi wa Shule ya Sokoine Memorial High School mkoani Morogoro.
Waziri alikuwa akikagua miradi inayotekelezwa katika halmashauri na kubaini dosari kwenye manunuzi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Amesema, Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, lakini kumekuwa na dosari katika suala zima la manunuzi inayosababisha miradi kukwama na kutomalizika kwa wakati.
Ameendelea kufafanua kuwa kumekuwa na dosari kwenye kunukuu bei kabla ya kupatiwa idhini na Mkurugenzi wa Halmashauri ambapo bei inatolewa halafu idhini inafuata baadaye jambo ambalo halikubaliki katika sheria za manunuzi.
Waziri Bashungwa amesema kuwa, dosari nyingine ni kuletwa kwa mzigo kwanza ndipo 'local purchasing order' inasiniwa ambapo ni kinyume na utaratibu pia utumiaji wa fomu za vivuli badala ya fomu halisi.
Ameendelea kufafanua kuwa, dosari nyingine kwa upande wa manunuzi ni kuwa upo ushahidi unaonesha uteuzi wa wazabuni kupewa kazi wakati hawakujaza fomu wakati wa kutafuta mzabuni, hivyo kuonesha kuwa kuna udanganyifu upande wa manunuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Aidha, amewaagiza Wakurugenzi wote nchini kufuata sheria kanuni na taratibu za manunuzi katika kuendesha halmashauri ili wasiingie kwenye matatizo ambayo yanatokana na kwenda kinyume na utaratibu.