NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema kuwa, Sekta ya Barabara kupitia Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mijini (TARURA) hazijaachwa nyuma badala yake Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeongeza nguvu zaidi ya kifedha.
Amesema,Serikali imetoa shilingi bilioni 597.00 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara za wilaya zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mijini (TARURA).
Mheshimiwa Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Machi 1,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani.
Amesema, fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 213.36 ikiwemo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilomita 1,152.33 nchini.
"Pia ni kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 25,059.4, ujenzi wa madaraja 201 ambapo ujenzi unaendelea ikiwemo ujenzi wa maboksi kalavati 70 na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 123.05,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.
Pia amesema, katika sekta ya barabara shilingi bilioni 430.88 zinatarajiwa kutolewa kwa kipindi cha kuanzia Machi hadi Juni, 2022 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara za wilaya zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara wa Vijijini na Mijini (TARURA).
Amesema, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 257.20, barabara kwa kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilomita 12,511.06, matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 2,945.08 na ujenzi wa madaraja 81 nchini.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TARURA wakipita kwenye daraja la mawe Kurugongo linalounganisha vijiji vya Kurugongo na Titye lenye urefu wa mita 22.4 likiwa limefikia hatua za mwisho kukamilika katika ziara ya ukaguzi wa miradi hivi karibuni katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.