Waziri Bashungwa: Utoaji wa mikopo asilimia 10 ya halmashauri umeimarika

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema kuwa, utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kutokana na Mapato ya Ndani ya Halmashauri, umeendelea kuimarika nchini baada ya kutungwa kwa sheria inayosimamia utoaji wa mikopo hiyo.
Mheshimiwa Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Machi 1,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan madarakani.

Amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, inasimamia utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya Ndani ya Halmashauri.

"Mikopo hii imekuwa ikitolewa kwa kipindi kirefu. Baada ya kuwepo changamoto mbalimbali, mwaka 2018/19 Serikali kupitia Sheria ya Fedha, ilirekebisha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 na kuongeza Kifungu cha 37A, ambapo kinahusu usimamaizi wa Utoaji wa Fedha za Mikopo, inayotokana na asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri. Mwaka 2019, zilitungwa Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo hii, na mwaka 2021 kanuni zilifanyiwa marekebisho,"ameeleza Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/19 hadi Januari 2022, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeweza kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 164.16, kwa vikundi 38,573 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

"Kati ya vikundi hivyo, vikundi 23,944 ni vya wanawake, vikundi 11,528 ni vya vijana, na vikundi 3,101 ni vya watu wenye ulemavu. Zaidi ya ajira 390,000 zimezalishwa kutokana mikopo hii,"amesema Waziri Bashungwa.

Pia amesema, katika kipindi hicho mamlaka za Serikali za Mitaa, zimeweza kukusanya marejesho yanayotokana na mikopo, zaidi ya shilingi bilioni 81, ambazo zimetumika kukopeshwa tena katika vikundi 46,610, ambapo vikundi 29,057 ni vya Wanawake, 14,383 ni Vijana na vikundi 3,170 ni vikundi vya Watu wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema,katika kipindi cha kuanzia Machi hadi Juni, 2022 kiasi cha shilingi bilioni tano zinatarajiwa kutolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu na mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wakiwemo Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.

Mapato ya Ndani ya Halmashauri

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri nchini kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2021/22, kwa kipindi cha Julai hadi Disemba, Waziri Bashungwa amesema kuwa, hali imeonesha ongezeko la makisio na makusanyo.

Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2018/19, makusanyo halisi yalikuwa shilingi bilioni 661.69; kwa mwaka wa fedha 2019/20, makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 717.24; mwaka wa fedha 2020/21, makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 757.05 na kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2021, makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 460.16 kati ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 863.85.

"Kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2021 hadi Januari, 2022 halmashauri zimekusanya kiasi cha shilingi bilioni 528.64 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 863.85. Aidha, katika kipindi cha kuanzia Februari hadi Juni, 2022, halmashauri zinatarajia kukusanya Shilingi bilioni 335.21,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news