Waziri Bashungwa:Utekelezaji operesheni anuani za makazi imefikia asilimia 67

*Zoezi kutamatika Mei 22,mwaka huu kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMO), Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema kazi ya utekelezaji operesheni ya anuani za makazi kwenye mikoa yote Tanzania Bara imefikia asilimia 67 ya utekelezaji wake.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma leo wakati wa kikao kazi kati ya Wakuu wa Mikoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kuhusu uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa operesheni ya anuani za makazi nchini.

“Tumefikia asilimia 67, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya, sina shaka na wakuu wa mikoa, ninaamini hili la operesheni ya anuani za makazi mtafanya vizuri,”amesema Waziri Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema, kwa sasa kazi iliyobakia ni kuongeza hamasa kwenye kazi hiyo na kutoa elimu kwa wananchi ili kazi hiyo iendelee vizuri na kufikia malengo yanayotarajiwa na Serikali.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, zoezi la utekelezaji wa operesheni ya anuani za makazi limekwenda vizuri na linatarajiwa kukamilika kabla ya muda uliopangwa ambao ni Mei 22, 2022 ikiwa ni pamoja na kukamilisha mfumo wenyewe wa anuani za makazi ambao upo chini ya wizara yake.

Waziri Nape amesema, kwa sasa Serikali inaendelea kutambua maoni yaliyotolewa, kutoa elimu kwa wananchi, kuandaa taarifa, kutengeneza taarifa hizo na kuziingiza kwenye mfumo ikiwa ni pamoja kuuweka mfumo wenyewe ili ufanye kazi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof.Riziki Shemdoe amesema, lengo la kikao kazi ni kujadili namna ambavyo wakuu wa mikoa wanaendelea kutekeleza operesheni ya anuani za makazi Tanzania Bara na kuwa kazi hiyo inakwenda sambamba na Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwezi Agosti, 2022.

Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema zoezi la anuani za makazi linaendelea vizuri kama ambavyo wizara iliwapa maelekezo kwani fedha za kazi hiyo zilipokelewa ijapokuwa kuna maeneo machache ambayo yalikuwa na tatizo la kimtandao wakati wa kutumia fedha za kazi hiyo.

Amesema, baadhi ya changamoto zilijitokeza ni wingi wa watu kwa baadhi ya mikoa pamoja na maeneo makubwa ya makazi, lakini wanashukuru wizara zilituma timu za wataalam katika kusaidia utekelezaji wa kazi hiyo.

Zoezi la anuani za makazi linafanywa na wizara mbili kwa pamoja ambazo ni Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ambalo linatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 22,mwaka huu kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akilizindua mnamo Februari 8, mwaka huu

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news