*Utaratibu wa wanafunzi kubadilisha machaguo yao utafanyika kuanzia Machi 30, 2022 hadi Aprili 19, 2022
NA OR- TAMISEMI
SERIKALI imetoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya tahasusi (combination) na kozi mbalimbali walizozichagua kupitia fomu ya Selform.
Hayo yamebainishwa leo Machi 30,2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, fursa hii ya siku 21 itamuwezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne 2021 yanayotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Amesema, pia baadhi ya wanafunzi hawakujaza kwa uhakika tahasusi au kozi zao kutokana na kutokuwa na uhakika wa ufaulu katika masomo yao.
"Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa mara nyingine tena inatoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne, mwaka 2021 kubadili machaguo yao ili kutoa mwanya zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu fulani katika maisha yake ya baadaye kwa namna ambayo anatamani yeye mwenyewe au kwa kushauriwa na wazazi au walezi wake sambamba na kadiri ya ufaulu wake kwa mujibu wa matokeo yalivyotoka,"amesema.
Mhe. Bashungwa amesema, utaratibu wa wanafunzi kubadilisha machaguo yao utafanyika kuanzia Machi 30, 2022 hadi Aprili 19 huku akisisitiza kuzingatiwa kwa muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa.
Amesema, wanaotaka kubadili machaguo wanatakiwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS) unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz.
"Ili mhitimu aweze kuingia kwenye mfumo itabidi kutumia Namba ya Mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2021, Jina Lake la Mwisho, Mwaka wa Kuzaliwa na Alama ya Ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa."
"Huduma hii ya kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi watapata changamoto, wawasiliane na Dawati la Huduma la Mteja kupitia barua pepe helpdesk@tamisemi.go.tz au kuwasiliana moja kwa moja na Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa simu +255 262 160 210 na +255 735 160 210 au kufika Ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa."
Aidha, Bashungwa amewataka wahitimu kutumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha machaguo Tahasusi ili waweze kusoma tahasusi au kozi ambazo wamefaulu vizuri ama wana malengo nazo zaidi.
"Mzazi ana nafasi ya kushiriki katika zoezi hili kwa kushauriana na mtoto wako katika machaguo yake. Tafadhali mzazi kubaliana na mtoto katika machaguo yake ili baada ya zoezi la uchaguzi pasiwepo malalamiko yoyote ya kwamba mtoto amepangiwa machaguo ambayo hakuyachagua,"amesema.
Aidha, Bashungwa amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imekamilisha utaratibu wa awali wa kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye fomu za Selform za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.
Uchambuzi wa matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha nne (CSEE) mwaka 2021 unaonyesha kuwa Watahiniwa wa Shule 422,388 sawa na asilimia 87.30 kati ya watahiniwa 483,820 wenye matokeo ya Kidato cha Nne wamefaulu ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.46 ikilinganishwa watahiniwa 373,958 wa mwaka 2020.