NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Maendeleo ya Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Doroth Gwajima ametaka mabaraza ya uwezeshaji wanawake kiuchumi yaanzie ngazi ya kata ili kuwainua kuanzia chini.
Ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa Tamasha la Mwanamke wa Pwani la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Machi 8, mwaka huu.
Gwajima amesema kuwa, mabaraza hayo ambayo kwa sasa yako ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa huku ngazi ya kata yakiwa hayana nguvu sana yamefanya vizuri ambapo wanawake waneweza kujiinua kiuchumi.
"Tumpongeze Rais wetu wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan kwa kuyaasisi mabaraza haya na kuyawezesha kwa kuyapatia fedha na yameleta mabadiliko makubwa kiuchumi kwa wanawake ifike wakati sasa yaanzie ngazi ya kata,"amesema Dkt.Gwajima.
Amesema, mabaraza ya wanawake yanapaswa kusimamiwa na majukwaa hayo yaanze ngazi ya kata kwa nchi nzima chini ya usimamizi wa Halmashauri na mikoa ili manufaa yaanzie ngazi ya chini kabisa ili kuleta maendeleo kwa wote.
"Nimesikia mpango wenu kutokana na mafanikio ya baraza lanu la mkoa mnaongelea kufungua kiwanda hili ni jambo kubwa sana na Pwani siyo ya kucheza ngoma na mdundiko ya sasa imebadilika haya ndiyo mawazo tunayoyataka,"amesema Dkt.Gwajima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa Rais ameonesha uwezo wa mwanamke katika ukombozi kwao.
Kunenge amesema kuwa, kwa sasa watoto wa kike wa mkoa wa Pwani wanapata elimu na hata kama akichezwa ngoma bado atapata elimu kwani mila na desturi ni muhimu ngoma siyo kweli ni majembe kwa sasa mila ha desturi ni muhimu lakini elimu ni muhimu zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani, Farida Mgomi amesema kuwa wanawake wamenufaika sana na wana kila sababu ya kumshukuru Rais kwa kazi kubwa anayoifanya.
Mgomi amesema kuwa, wao kama viongozi wa chama na Serikali watamuunga mkono kwa kumkwamua mwanamke kiuchumi na kuhamasisha kujiunga na majukwaa hayo ya kiuchumi ili kila mwanamke uchumi wake.
Tags
Habari