Waziri Dkt.Jafo aunda Kamati ya Kitaifa ya watu 11 kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji Mto Mara

NA FRESHA KINASA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Dkt. Suleiman Jafo (Mb) ameunda Kamati ya Kitaifa ya watu 11 kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa maji ya Mto Mara.
Akizungumza leo Machi 12, 2022 baada ya kutembelea Mto Mara katika eneo la Kirumi na kupokea taarifa kutoka kwa viongozi, wananchi na wataalamu, Mheshimiwa Jafo ameitaka kamati hiyo kufanya uchunguzi wa maji ya mto huo na kutoa taarifa ndani ya kipindi cha siku saba kuanzia leo.

Mheshimiwa Jafo, amesema mbali na kufanya uchunguzi wa maji ya Mto Mara pia, ifanye uchunguzi wa maji yote kandokando ya mto huo ili kuona kama kuna uchafuzi wa namna hiyo na kutoa mapendekezo ya kitaalam ili kukabiliana na uchafuzi huo katika Mto Mara.
Mheshimiwa Jafo amesema kuwa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Prof. Samwel Manyele, kutoka Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Katibu wa Kamati hiyo ni Dkt. Samuel G. Mafwenga, Mkurugenzi Mkuu, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Dkt. Kessy F. Kilulya, Mkuu wa Idara ya Kemia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Charles Kasanzu, kutoka Idara ya Jiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bwana Daniel Ndio, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali, Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Bwana Renatus Shinhu, Mkurugenzi wa Bonde, Mamlaka wa Bonde la Maji Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Jafo amewataja wajumbe wengine kuwa ni Baraka Sekadende, Mkurugenzi wa Kituo, Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), Mwanza, Dkt. Neduvoto Mollel, kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Usimamizi wa Viatilifu (TPHPA), Afisa kutoka Ofisi ya Rais Ikulu, Bwana Yusuf Gobe Kuwaya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Faraja Ngelageza, Mkurugenzi Msaidizi Bioanuai, kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Jafo amesema kutokana na uchafuzi huo, maji yamebadilika rangi, yanatoa harufu na samaki aina ya sato wamekuwa wanakufa na kuelea katika mto huo.

Mheshimiwa Jafo amewataka wananchi, Serikali na wadau wote kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati hiyo katika kipindi chote watakachokuwa wanafanya uchunguzi wa jambo hilo.

Pia, Mheshimiwa Jafo ameitaka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutafuta mbadala wa upatikanaji wa maji kwa wananchi waliopo kandokando ya mto Mara wakati uchunguzi ukiwa unaendelea kufanywa juu ya jambo hilo.

Mkutano wa Mheshimiwa Jafo ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelis Mafumiko, Wakuu wa Wilaya za Rorya, Tarime na Butiama, wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zinazohusiana na Maji, Mazingira na Barabara.

Juma Peter ni mkazi wa eneo la Kirumi ambapo amesema, hatua ya Serikali kuchukua hatua za haraka juu ya Jambo hilo, inamanufaa makubwa kwa wananchi ambao wamepatwa na hofu juu ya hali hiyo.
"Hali hii imetutisha sana mto Mara kuchafuka na viumbe wakiwemo samaki kufa na kuelea juu, lakini naishukuru Serikali kufika na kuchukua hatua ambazo zinatija kwa wananchi na maisha yao kwa hakika serikali inatujali wananchi wake,"amesema Peter.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news