NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara (Mb), Mhe. Dkt.Ashatu Kijaji amewaasa watendaji na wananchi kwa ujumla kuwa tayari kuwapokea wawekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) waliosaini mikataba 37 yenye thamani ya takribani trilioni 20 na ajira zaidi ya 200,000, ambao wanatarajiwa kuingia nchini kuanzia wiki ya pili ya mwezi Machi 2022 kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano hayo bila kuwakwamisha katika ngazi yeyote husika.
Aidha, Dkt. Kijaji amefafanua kuhusu hati hizo 37 zilizofanyiwa uchunguzi na kupitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kutiwa saini kati ya wawekezaji kutoka UAE na Tanzania katika sekta mbalimbali za kiuchumi kuwa zinajumuisha Hati za Makubaliano katika Sekta ya Kilimo (11), Nishati nane (8), Usafirishaji tano (5), Mawasiliano nne (4), Ujenzi tatu (3), Madini mbili (2), Miundombinu moja (1), Maliasili moja (1), Afya moja (1) na Viwanda moja (1).
Dkt. Kijaji pia amesema Serikali imeandaa Mkakati wa utekelezaji wa uwekezaji wa Hati hizo za makubaliano kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinazohusika pamoja na Sekta Binasfi. Aidha, Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania kinachojumuisha Ofisi zote muhimu zinazohusika katika uwekezaji katika sehemu moja kimeanza kufanya usajili wa makampuni ya wawekezaji hao.
Vilevile, Waziri Kijaji alisema kuwa Tanzania imepata fursa ya kutangazwa katika jengo refu kuliko yote Duniani liitwalo Burj Khalifa lililopo katika Jiji la Dubai, kwa muda wa mwezi mzima wa Machi, 2022 bila gharama yoyote ambapo picha za vivutio mbalimbali vya Tanzania vitatangazwa katika jengo hilo.