Waziri Dkt.Mabula aanika mafanikio ya Sekta ya Ardhi mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani

>Shirika la NHC laruhusiwa kukopa Bilioni 173.9 /- kwa ajili ya kukamilisha miradi yake

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

WAKATI Serikali ya Awamu ya Sita ikielekea kutimiza mwaka mmoja madarakani Machi 19, 2022 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ameanika mafanikio ya serikali hiyo.

Ni katika kipindi cha mwaka mmoja katika sekta yake na kueleza kuwa sekta hiyo imepiga hatua kubwa katika masuala mbalimbali ikiwemo usajili wa hati na kuongeza kasi ya upimaji ardhí nchini.

Aidha, Dkt.Mabula amesema, Serikali ya Mhe.Samia pia imeiwezesha wizara yake kupitia miradi mbalimbali kuhakikisha inapanga, inapima na kumilikisha ardhí nchini.
Akizungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa wizara yake leo Machi 8,2022, Dkt.Mabula amesema, katika kipindi cha mwaka mmoja Wizara ya Ardhi imeweza kupatiwa shilingi Bilioni 50 kama mkopo kwa ajili ya Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika halmashauri mbalimbali nchini.

Mbali na kiasi hicho, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan pia imeiwezesha Wizara ya Ardhi kupatiwa kiasi cha shilingi Bilioni 345 na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha Milki za Ardhi nchini

‘’Kwanza niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wizara yangu shilingi Bilioni 50 kwa ule mradi wa KKK pamoja na Bilioni 345 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha milki za ardí, fedha hizi zitatusaidia sana kuboresha milki za ardhí hasa ikizingatiwa ni asilimia 25 tu ardhí yote ya Tanzania ndiyo imepimwa,’’amesema Dkt.Mabula.

Mafanikio mengine ni pamoja na kusajiliwa Hatimiliki 41,533 pamoja na Hati za Sehemu ya Jengo 161 sambamba na kusajiliwa Hatimiliki 3,735 za kielektroniki kupitia mfumo wa ILMIS.

Aidha, Dkt.Mabula amebainisha kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja wizara yake iliweza kukamilisha kazi mbalimbali za uthamini ikiwemo uthamini wa mali za wananchi kwenye ujenzi wa barabara ya pete (Ring Road) jijini Dodoma wenye thamani ya shilingi bilioni 12.76 na ule wa Kijiji cha Fella wilayani Misungwi kupisha ujenzi wa kambi (camping site) ya Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa SGR Lot V.

"Pamoja na kazi kubwa iliyofanyika kwenye suala la utahmini, wizara imekamilisha pia majedwali ya fidia ya mali za wananchi 1,525 katika mkuza wenye urefu wa kilomita 89 ambapo shilingi 3, 818, 123,062 zitalipwa kama fidia kwa waathirika,’’amesema Dkt.Mabula.

Ameongeza kwa kusema kuwa, wizara yake pia iliweza kutatua migogoro ya ardhí 745 katika mikoa na halmashauri mbalimbali nchini kupitia Programu ya Funguka kwa Waziri huku ikifanikiwa kukusanya shilingi 119,501,946.6 kupitia kodi ya Pango la Ardhi.

Kuhusu upimaji ardhi, Waziri Dkt.Mabula amesema, Wizara ya Ardhi ilifanikiwa Kupima na Kuidhinishwa viwanja 232,599 pamoja na mashamba 353 huku ikinunua ndege ndogo isiyo na rubani (drone) kwa ajili ya kupiga picha za anga zitakazowezesha uandaaji wa ramani za msingi.

Pia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ilitoa shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Kenya.

Katika kuhakikisha Wizara ya Ardhi inashughulikia kero za wananchi kwa haraka, Dkt.Mabula amesema, wizara yake imeanzisha Kituo cha Mawasiliano kwa Wateja (Call Centre) Ofisi ya Makao Makuu ya wizara jijini Dodoma kwa lengo la kuondoa chanagamoto katika sekta ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, katika kipindi cha mwaka mmoja Wizara ya Ardhi ilifanikiwa kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji 51 vinavyopitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika Halmashauri za Singida (8), Iramba (5), Muheza (12), Kilindi (8), Nzega (12) na Chemba (6).

Akigeukia upande wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, alisema katika kuboresha utendaji kazi wa Mabaraza ya Ardhi, wajumbe 151 waliteuliwa sambamba na kuanzishwa Mabaraza mapya ya Mbarali na Nkasi na kufanya idadi ya Mabaraza kuwa 60.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi (wa pili kushoto) akipata maelezo kuhusiana na mradi wa ujenzi wa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Chamwino kutoka kwa msimamizi wa ujenzi, Grace Musita wakati alipotembelea miradi ya NHC ya Iyumbu na Chamwino jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa NHC, Dkt.Maulid Banyani.

‘’Pamoja na maboresho kwenye mabaraza ya ardhi lakini pia tumerekebisha Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura ya 216 ili kuwezesha Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuwa na ajira za kudumu badala ya ajira za mikataba,"amesema Dkt.Mabula.

Kwa upande wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Dkt.Mabula amesema, Serikali ya mama Samia imeliwezesha shirika hilo kupata fedha za kukamilisha miradi yake mbalimbali iliyosimama pamoja na ile ya kimkakati.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa, ni machinjio ya kisasa ya Vingunguti mradi uliogharimu shilingi bilioni 12.5 ambayo ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 1,500 na mbuzi 1,000 kwa siku, Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa, Manispaa ya Musoma inayogharimu shilingi bilioni 17.2 na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliyojengwa Mtwara eneo la Mikindani na kugharimu shilingi bilioni 15.8.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi amekutana na waandishi wa habari kwenye eneo la mradi wa ujenzi wa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Iyumbu sambamba na kutembelea mradi wa nyumba wa Chamwino jijini Dodoma.

Katika mkutano huo Dkt.Kijazi amesema, Shirika la Nyumba limeandaa mikakati kuhakikisha linakwamua miradi yote ya shirika hilo iliyosimama ikiwemo ya Morocco Square na Kawe.

Alibainisha kuwa, katika kufanikisha suala hilo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeliruhusu shirika hilo kukopa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 173.9 kwa ajili ya kukamilisha miradi yake ikiwemo ya Morocco Square, Kawe pamoja na Plot 300 Regent.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Dkt.Maulid Banyani (kulia) akifafanua jambo mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Allan Kijazi wakati Katibu Mkuu alipotembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za NHC Chamwino mkoani Dodoma leo Machi 8, 2022. Kushoto ni Msimamizi wa ujenzi huo, Grace Musita.

Dkt.Kijazi alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kubuni miradi ya ujenzi kwa kutumia wataalamu wa ndani na kubainisha kuwa ubunifu huo umelifanya shirika kuingia kwenye ushindani wa ndani na nje katika masuala ya ujenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news