NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa jijini Tanga.
Miradi aliyoitembelea na kukagua hatua za ujenzi wake ni pamoja na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Jeshi na maabara ya mafunzo.
Mradi wa uboreshaji wa uwanja wa ndege unajumuisha ujenzi wa karakana ya ndege, mitaro ya maji ya mvua, uzio kuzunguka uwanja huo, nyumba ya Mlango Mkuu wa Kiteule cha Shule ya Anga ya Kijeshi (SAK).
Unatekelezwa kwa mieizi sita ambapo ujenzi wake ulianza tangu Novemba, 24 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 24,2022. Mradi utakapokamilika utakuwa umegharimu jumla ya sh.bilioni 1.8.
Pia Dkt.Tax alitembelea mradi wa maabara ya mafunzo katika Shule ya Kijeshi ya Ulinzi wa Anga (SKUA) iliyopo jijini Tanga.
Miradi yote miwili inatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya SUMAJKT (SUMAJKT Construction Company Limited) Kanda ya Kaskazini akiwa ni mkandarasi, Mshitiri ni Wizara ya Ulinzi na JKT na Mshauri Mwelezi ni MOD Consulting Unit ambacho ni kitengo chini ya wizara.