NA VERONICA MWAFISI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema wakulima 2,409 na Vyama vya Ushirika vitano wamewezeshwa kukopa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 28.2 kupitia hatimiliki za ardhi zilizotolewa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Baadhi ya watumishi wa MKURABITA wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na watumishi wa MKURABITA alipofanya ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Mhe. Jenista amesema kuwa, mikopo hiyo imewawezesha wakulima hao kuingia kwenye kilimo bora na cha kisasa ambacho kinaliwezesha taifa kuwa na akiba ya hifadhi ya chakula cha kutosha.
“Mikopo hiyo imewasaidia pia wakulima kuondokana na ukulima wa kawaida na kuingia kwenye kilimo cha biashara ambapo anakuwa ni mlipa kodi mzuri anayechangia ukuaji wa uchumi,” Mhe. Jenista amefafanua.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, wamiliki 206 waliorasimisha viwanja maeneo ya mjini wametumia hatimiliki kupata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.
Akimkaribisha Mhe. Waziri kuzungumza na watumishi, Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe amesema wakulima hao 2409 waliotumia Hatimiliki za ardhi kupata mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 28.2 wamethibitisha wenyewe kwa maandishi kupitia fomu walizojaza.
Aidha, Dkt. Mgembe amesema, wafanyabiashara waliopata mafunzo kupitia MKURABITA wameweza kukopa zaidi ya shilingi bilioni 9.38 kwa ajili ya kuongeza mitaji ya biashara zao.