*Apongezwa kwa ubunifu, aongoza kipindi cha Aridhio cha TBC, asoma habari, afanya mahojiano na Waziri Mkuu Majaliwa, Dkt. Yonazi
NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape Nnauye na Katibu Mkuu wake, Dkt. Jim Yonazi leo wameonesha ubunifu mkubwa na uongozi baada ya Mhe. Nape kusoma taarifa ya habari ya TBC ya saa mbili kamili usiku ya Aridhio kwa umahiri mkubwa.
"Haijawahi kutokea kumuona Waziri na Katibu Mkuu wake wakisoma habari na kufanya mahojiano," amesema Mtazamaji wa TBC Halfan Mahfudh, akitoa pongezi lukuki.
Nape ambaye ni mwanahabari nguli, alimwalika Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Yonazi, ambaye alimhoji na kuelezea mafanikio makubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan chini ya Wizara hiyo, hasa katika utekelezaji wa zoezi la anuani za Makazi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Dkt. Yonazi ambaye, kabla ya uteuzi wake kama Naibu Katibu Mkuu, alikuwa Mhariri Mtendaji katika Kampuni ya Magazeti ya Serikali, TSN na kuiongiza taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa, pia ni Mtaalamu mbobezi wa Teknolojia ya Habari (IT).
Mhe.Nape ambaye amewashangaza wengi kwa umahiri wa kusoma habari, huku akiweka historia kama Waziri kuonesha uongozi kwa kusoma habari katika televisheni ya umma, baadaye alimwalika Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu umuhimu na mafanikio ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia kuhusu anuani za makazi nchini.
Amempongeza Rais Samia kwa azma ya kuibadilisha Tanzania iingie katika ustaarabu wa anuani za makazi ambao utasaidia kuimarisha biashara ya mtandaoni (e-commerce).
Alisema sekta ya usafiri wa mijini kama Bajaj, Boda au Teksi, pia itaimarika na kufanya Nazi kwa ufanisi mkubwa, hivyo kutengeneza ajira zaidi.
Watazamaji wa TBC wametoa pongezi kwa Mhe Nape na Dkt Yonazi kwa ubunifu mkubwa na uongozi.
"Kwa mtaji huu, Tasnia ya habari itarajie mageuzi makubwa ya kisera na kiutendaji," amesema Faith Masha wa Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, kuongoza ni kuonesha njia, viongozi hawa wametoka ofisini mwao na kufanya kila wanachohimiza majukwaani.