NA MWANDISHI MAALUM
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi ameagiza miradi yote ya Wizara ya Afya chini ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) iwe imekamilika kabla ya Juni 30, 2022.
Prof. Makubi ameyasema hayo mkoani hapa alipotembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya mkoa huo,
"Naagiza nchi nzima miradi yote ya IMF kwenye sekta ya afya inayosimamiwa na wizara ya afya iwe imekamilika Juni 30,2022, nje ya hapo ni kukaidi maagizo ya viongozi na masharti ya matumizi ya fedha hizi na tutakuondoa,"amesema.
Aidha, Prof. Makubi amewataka uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kukaa na mkandarasi, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa, Mshauri elekezi na Watalaamu wa Majengo toka Wizara ya Afya kuhakikisha mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kabla ya mwezi wa sita kuisha,
"Kakaeni pamoja, ule mradi watu wafanye kazi saa ishirini na nne , mkandarasi aongeze wafanyakazi , waweke taa za usiku wafanye kazi usiku na mchana ili wakabidhi kabla ya mwezi wa sita haujaisha,"amesisitiza Prof.Makubi.
Kwa upande mwingine, Prof. Makubi amewapongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kufanya vizuri kitaifa katika eneo la chanjo dhidi ya UVIKO-19.