NA DOREEN ALOYCE
NAIBU wa Waziri wa Maji,Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaaban Ali Othman ametoa onyo kali kwa yeyote atakayekiuka sheria za uvunaji wa rasilimali za nchi hususani mchanga kwani atachukuliwa hatua ikiwemo kuwajibishwa bila kujali cheo chake.
Pia ametahadharisha baadhi ya watendaji wa wizara hiyo ambao wanahusika kujua wanaofanya vitendo hivyo vya uvunaji holela wa rasilimali na kunyamaza jambo ambalo halitafumbiwa macho.
Amesema, semina hiyo ni baada ya kubaini kuwa kuna uelewa tofauti kwenye maeneo yale ya kiutawala hasa wizara inapopanga taratibu zake na utekelezaji haufanikiwi kadri ilivyokusudia.
Aidha, amesema kutokana na kinachoendelea hasa cha uvunjifu na ukiukwaji wa taratibu katika maeneo yao hasa uvunaji wa rasilimali mchanga wakaona ni vyema wakae pamoja ili wawe na mwelekeo wa mmoja namna ya kudhibiti rasilimali hizo.
"Wizara tumejipanga kusimamia hilo, hatutamfumbia macho atakayebainika kuvunja sheria, niwaombe warudi katika mfumo ambao umewekwa kisheria na sio vinginevyo lengo ni kuvuna na kuratibu na hatimaye kuwa na uelekeo mmoja kama Serikali.
"Nakuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara kuhakikisha kamati zitakazoundwa na wakuu wa wilaya yao watakaounda kamati za kutusaidia sisi kukamata rasilimali hizo na kuletwa hapa wizarani na wale wa kupigwa faini, wapigwe ili wapewe asilimia ili kuweka motisha kwao kutokana na gharama walizozitumia,"amesema.