NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WAAMUZI na walimu wa mchezo wa mpira wa pete nchini wametakiwa kutumia taaluma zao kuibua vipaji vya vijana vijijini.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Gerald Mwarekwa kutoka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) wakati wa kufunga mafunzo ya walimu na waamuzi.
Mwarekwa amesema kuwa, mafunzo hayo yatasaidia kuongeza vipaji pia kuendana na Dunia inavyotaka ambapo moja ya changamoto kubwa kwenye michezo ni waamuzi na walimu.
"Haya ni mafunzo mazuri sana hapa wanatoka na ujuzi na maarifa na muende na kuwasaidia vijana ili matunda yaonekana na mafunzo yalete tija, kwani mmeiva nendeni huko hata vijijini,"amesema Mwarekwa.
Amesema kuwa, wanarudi kazini hivyo watumie muda kutoa maarifa, "matokeo tunakwenda kuyatumia ili kuuibua mchezo huu, michezo ni ajira kubwa kule kuna vipaji vingi muende kuibua vipaji,"amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Netiboli (CHANETA) Taifa, Devotha Marwa amesema, mafunzo hayo yatasaidia kuleta chachu ya mchezo huo na wataibua na kuendeleza vijana.
Naye ofisa michezo Mkoa wa Pwani, Grace Bureta amesema mafunzo hayo wanapaswa kuyafanyia kazi ili kuwapatia ujuzi wana michezo ambapo kwenye michezo ya Umitashumta na Umiseta kutakuwa na vitu vya tofauti.
Tags
Michezo