NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KLABU ya Yanga SC imeendelea kuonesha ubabe katika michuano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya leo kuzitumia dakika tisini kwa kuzoa alama zote tatu kupitia bao moja wakiwa ugenini.
Mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele ndiye aliyewapa raha Wanajangwani na kuharibu mipango ya Geita Gold ambao walionekana kuwa na shauku ya kupata ushindi.
Kupitia mtanange huo uliopigwa katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza Mayele ambaye yupo katika msimu wake wa kwanza Yanga tangu asajiliwe kutoka AS Vita ya kwao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alifunga bao hilo sekunde ya 33 dakika ya kwanza.
Mayele alionekana kutumia vizuri makosa ya walinzi wa Geita Gold ambapo bao hilo lilidumu hadi dakika 45 za kwanza.
Aidha, kipindi cha Pili Geita Gold walirejea kwa kasi kutafuta bao la kusawazisha na kutengeneza nafasi kadhaa, lakini kukosekana kwa umakini kwa washambuliaji wao na uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga uliwanyima nafasi ya kupata bao la kusawazisha ili kupata angalau alama moja katika dimba lao la nyumbani.
Hata hivyo, benchi la ufundi la Yanga lilifanya mabadiliko kadhaa kuimarisha eneo la kiungo, Denis Nkane na Paul Godfrey walitolewa na nafasi zao kuchukuliwa na Zawadi Mauya na Dikson Ambundo.
Pia baadae mshambuliaji Fiston Kalala Mayele alipata majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na Heritie Makambo.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha alama 45 katika mchezo wa 17 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu ya NBC kwa alama 11 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.
Wakati huo huo, Geita Gold baada ya kichapo cha leo wanabaki na alama zao 21 za mechi 17 sasa katika nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu ambao kila mmoja anatamani kuwa mbele ya mwingine kutokana na ukubwa wake kwa sasa.