NA DIRAMAKINI, Handeni
MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga,Siriel Mchembe ametoa siku saba kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia na Rushwa (TAKUKURU) na Idara ya Ukaguzi Halmashauri Mji Handeni kufuatilia na kuchunguza tuhuma 20 zinazomkabili Mtendaji wa Kata ya Misima, Athumani Mgaza.
Licha ya maagizo hayo kwa taasisi hizo,pia mkuu huyo wa wilaya ameagiza kusimamishwa kazi kwa mtendaji huyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo 20 zinazomkabili.
Mchembe amesema hayo kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza wananchi na viongozi wa Mtaa wa Bwila kutokana na madai ya kutoshirikishwa kwenye ujenzi wa zahanati na kusema kuwa, mtendaji huyo amekutwa na tuhuma ya makosa 20,hivyo kutakiwa kusimama kazi kupisha uchunguzi.
"Haiwezekani mtendaji wa kata kuwatisha wenzake wanapotoa taarifa,lakini anakesi ya ubadhirifu wa shilingi milioni 7, TAKUKURU na ameanza kuzirejesha baada ya kukiri makosa,pia anadaiwa kuwa na posi kama nne anazozitumia kujipatia fedha kitu ambacho ni kosa.
"Lakini aliwahi kusimamishwa kazi na baraza la madiwani kwa makosa mbalimbali ya kiutendaji kazi kutoka Kata ya Kwamagome,"amesema Mchembe.
Reuben Kwagilwa ambaye ni Mbunge wa Handeni Mjini alimuomba mkuu wa wilaya kuhakikisha watendaji wa serikali wanafanya kazi kwa kuzingatia maadili,pia kuwaonea huruma wananchi kwa shida wananzopata katika kukosa huduma.
Amesema, kwa mtumishi yeyote ambaye atabainika na makosa hatua kali za kisheria dhidi yake zichukuliwe,lengo ni ili iwe fundisho kwa wengine kwa tabia kama hizo.
Naye Athumani Mgaza ambaye ni Mtendaji kata ya Kwenjugo katika kikao hicho amesema, baadhi ya maamuzi ameyafanya kutokana na maagizo kutoka ofisi ya mkurugenzi,na sio maamuzi yake.