NA DIRAMAKINI
HUDUMA ya Al Barakah ya Benki ya CRDB inayozingatia misingi ya kutotoza au kupokea riba imewafurahisha wananchi, wadau na viongozi wa Mkoa wa Tanga.
Hilo limebainika katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wateja, wadau na wenye uhitaji katika Mkoa wa Tanga ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa benki hiyo kufuturisha kipindi cha mfungo wa Ramadhani.
Hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Tanga Beach Resort ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Sheikh Juma Luwuchu.Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mh. Hashim Mgandilwa akizungumza na wateja na wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tanga wakati wa futari ya Benki ya CRDB iliyofanyika katika hoteli ya Tanga Beach Resort.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa akishiriki futari na wateja na wadau wa Benki ya CRDB wa Mkoa wa Tanga.
Akizungumza katika futari hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Hazina na Masoko ya Mitaji wa Benki ya CRDB, Bw. Alex Ngusaru alisema kuwa Benki ya CRDB imeendelea kusikiliza maoni ya wateja na kuendelea kuleta sokoni bidhaa na huduma bunifu zinazoendana na mahitaji ya soko.
“Uanzishwaji wa huduma ya Al Barakah unadhihirisha ni kwa kiasi gani ambavyo Benki yetu inaishi kauli mbiu yake ya “Benki Inayomsikiliza Mteja” kwani kupitia kusikiliza maoni ya wateja wetu ndipo tulipoweza kuja na huduma hii makhususi kwa ajili ya wenzetu ambao wanaamini katika misingi ya kutopokea wala kutozwa riba” alisema Ngusaru.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Sheikh Juma Luwuchu akizungumza na wateja na wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tanga wakati wa futari ya Benki ya CRDB iliyofanyika katika hoteli ya Tanga Beach Resort.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mh. Hashim Mgandilwa ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga katika hafla hiyo aliipongeza na kuishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa futari hiyo kwa wakazi wa Tanga pamoja na kuandaa vyakula kwa ajili ya wenye uhitaji ili kuwasaidia katika kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Mkuu wa Wilaya aliongeza kuwa ujio wa huduma ya Al Barakah utakua chachu ya kuongeza wigo kwa kufikisha huduma za fedha kwa Watanzania kwani wapo ambao walikua hawawezi kutumia huduma za benki kwa kuwa tu haziendani na misingi ya imani yao.
“Nawapongeza sana Benki ya CRDB kwa hili la futari na kugusa wenye uhitaji lakini zaidi niwapongeze kwa kuja na huduma hii makhusi ya Al Barakah ambayo inaendana na imani ya wenzetu wasioamini katika kutozwa au kupokea riba,” alisema Mhe. Mgandilwa.
Wateja na wadau wa Benki ya CRDB Mkoa wa Tanga waliojitokeza kushiriki futari ya Benki ya CRDB iliyofanyika katika hoteli ya Tanga Beach Resort.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mh. Hashim Mgandilwa akiwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya CRDB, Bi. Chiku Issa (wa pili kushoto) wakikabidhi vyakula kwa kituo cha wenye uhitaji cha Imani Chumbageni ikiwa ni sehemu ya mchango wa Benki ya CRDB kwa kituo hicho katika mfungo wa mwezi Ramadhani.
Kwa upande wake Shekhe wa mkoa wa Tanga Juma Luwuchu ambae aliambatana na masheikh wengine wa Mkoa alitoa shukrani na pongezi kwa Benki ya CRDB kwa kuipa heshima Tanga kwa kuamua kuifanya kuwa moja kati ya mikoa ambayo benki itaandaa futari kwa mwaka huu lakini zaidi akifurahishwa na huduma ya Al Barakah inayofata misingi ya Sharia.
Sambamba na hilo Sheikh Luwuchu aliwaasa Waislamu pamoja na taasisi nyingine kuiga mfano wa Benki ya CRDB cha kukumbuka wenye uhitaji katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan huku akiwataka Waislamu kuhakikisha wanadumisha yale mema na mazuri yaliyoelekezwa katika Quran tukufu.
Wafanyakazi wanawake wa Benki ya CRDB wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kushiriki futari na wateja na wadau wa benki wa Mkoa wa Tanga.
“Benki ya CRDB wametuonyesha mfano mzuri kwa kuwakumbuka wateja na wadau wao lakini hawakuishia hapo wamekumbuka pia watoto wetu wenye uhitaji kutoka kituo cha Imani Chumbageni,” alisema Sheikh Luwuchu.
Kituo cha Imani Chumbageni ambao pamoja na kualikwa katika futari hiyo pia walikabidhiwa vyakula mbalimbali ikiwemo ngano, sukari, tambi, tende na mafuta ya kupikia ili kuwasaidia kupata futari kipindi cha mfungo wa mwezi Ramadhani.