NA DIRAMAKINI
WAANDISHI wa habari katika Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Simiyu (Simiyu Press Club-SPC) wametakiwa kuongeza kasi ya kuandika habari za uchunguzi katika mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza uhuru wa kujieleza.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw.David Kafulila katika mdahalo wa Uhuru wa Kujieleza uliofanyika Aprili 20, 2022 ambao umehusisha wadau mbalimbali wakiwemo Waandishi, Wanasheria, Jeshi la Polisi, Asasi za kiraia na za Kiserikali, pamoja na viongozi wa dini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Bw. Lupakisyo Andrea Kapange amewapongeza waandishi kwa kazi kubwa ya kupasha habari na kuwataka kuwa mabalozi wazuri katika kuutangaza Mkoa wa Simiyu kwa mambo mazuri ikiwemo kilimo cha pamba kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Simiyu (SPC), Bw. Frank Kasamwa akizungumza katika ufunguzi wa mdahalo huo, ameishukuru Serikali kwa kuboresha mahusiano mazuri na vyombo vya habari na kuomba ushirikiano huo uzidi kuimarika.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Klabu ya Wandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (Mwanza Press Club-MPC), Bw. Edwin Soko ambaye alikuwa muwasilishaji wa mada amewasihi wadau kuwa na utamaduni wa kujitokeza kushiriki midahalo ya namna hiyo kwani wao ndio chachu ya aidha kuminya au kutekeleza Uhuru wa Kujieleza.
Ameongeza kuwa Mwandishi wa Habari asipopata ushirikiano wa kupewa taarifa sahihi na za kutosha toka kwa mdau inapelekea kuua habari na hivyo jamii inakosa haki ya msingi ya kupata habari.
Mdahalo huo umeratibiwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) kwa kushirikiana na Shirika la IMS (International Media Support) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi katika mpango endelevu wa kuboresha Uhuru wa kujieleza kwa Waandishi wa Habari Nchini.