NA FRESHA KINASA
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Musoma mkoani Mara, Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila amewaasa waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kudumu katika kutenda matendo mema ikiwemo kuwasaidia watu wenye uhitaji na kujiepusha na vitendo viovu na vya kikatili, ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi.


Pia, Mhashamu Baba Askofu Msonganzila amewasisitiza waumini wa kanisa hilo, kuendelea kuitunza na kuithamini miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa na wafadhili iweze kudumu na kuwa na manufaa endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mradi wa kwanza ni hosteli ya ghorofa mbili kwa ajili ya wanafunzi 200 yenye vyumba 20 katika Shule ya Msingi Edmond Blessed. Jengo hilo limewekewa miundombinu ya kisasa inayowezesha upatikanaji wa huduma za maji na umeme na huduma zote muhimu.


Mradi wa pili ni kituo cha Afya chenye jina la Mvua na Jua Lengo Moja ambacho kimejengwa kisasa kikiwa na miundombinu ya kuteketeza taka, mifumo thabiti ya maji na Umeme wa jua ambao unaotosheleza mahitaji ya kituo katika kutoa huduma za matibabu.
Mradi wa tatu ni kituo cha kisasa cha kilimo na ufugaji chenye mabanda ya nguruwe, kuku, ng'ombe wa maziwa, trekta, mitambo mbalimbali na vifaa vingine kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

Aidha, amepongeza pia uongozi wa Parokia ya Kiabakari kwa kazi nzuri na ushirikiano walio nao na jamii hali ambayo imewezesha miradi iliyotekelezwa kufanyika kwa ufanisi mkubwa na kwamba, itakidhi malengo yaliyokusudiwa.
