NA FRESHA KINASA
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la New Life Gospel Community Church-Tanzania (Bonde la Baraka) nchini lenye makao makuu yake Kigera Bondeni Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara, Daniel Ouma amewataka Watanzania wajitokeze kushiriki kikamifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika mwezi Agosti, 2022 ili kuiwezesha serikali kupanga Mipango ya maendeleo.Askofu Ouma amesema kuwa, zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na wananchi wote. Hivyo amesisitiza Watanzania washiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu. Huku akisema viongozi wa dini zote washiriki kuhamasisha jambo hilo ili lifanikiwe kwa ufanisi.
Ameyasema hayo leo Aprili 17, 2022 wakati akihubiri katika Ibada ya Pasaka iliyofanyika kanisani hapo, ambapo pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo katika Mkoa wa Mara na maeneo mbalimbali nchini.
Sambamba na juhudi zake za thabiti za kuwaletea maendeleo Watanzania katika nyanja ya kijamii na kiuchumi.
"Niwaase Watanzania wote, tushiriki kwa kwa ufanisi, sensa ya mwaka huu itakuwa ya sita kufanyika baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana. Hakuna sababu ya mtu kuzuia watu wasihesabiwe, bali tuhimize watu wahesabiwe. Sensa hata makanisa zinafanyika wachungaji wanahesabu idadi ya mahudhurio ya washirika, nakazia lazima zoezi hili lifanyike vizuri sana bila kukwamishwa,"amesema Askofu Ouma.
"Sensa ina faida kubwa sana kwa nchi, Serikali itatambua hali za maendeleo ya wananchi, hali ya ajira, hali ya utoaji wa huduma za jamii, kupata takwimu sahihi na mambo mengine mengi ya muhimu kila kitu cha thamani kinahesabiwa na ndio maana fedha zinahesabiwa sembuse na binadamu ambaye thamani yake ni kubwa kuliko chochote,"amesema Askofu Ouma.
"Zipo sababu za Sensa kwani kila nambari ina thamani kubwa kwa Mungu, kuhesabu kunapatikana katika Biblia, tunasoma Yesu alilisha watu 5,000 hiyo tayari ni hesabu, mjane alihesabu sarafu, na katika Biblia kuna kitabu kinachoitwa Hesabu kwa hiyo wanaopotosha Sensa waache na wapuuzwe kwani nia yao si nzuri. Na katika michezo tunaona takwimu hutolewa zikionesha idadi ya mashuti yaliyolenga lango, umililiki wa mpira, idadi ya kona zilizochezwa, hizo zote ni hesabu. Na ndio maana Taifa lina mipango yake ya maendeleo,"amesema Askofu Ouma.
Aidha, Askofu Ouma amewataka Watanzania wote kuepukana na udini, ukabilia bali amesisitiza kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano, na pia akasisitiza kuheshimu Serikali na kuthamini mipango mbalimbali inayopangwa kwa maendeleo endelevu ya nchi na Wananchi pia.
"Sisi Watanzania tuna neema ya kipekee kutokana na msingi mzuri uliowekwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisistiza umoja, amani utulivu na upendo, tuendelee kuwa wamoja na kushikamana tukiunga mkono Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Hassan ambaye amekuwa mfano bora kwa uwajibikaji thabiti kwa manufaa ya Watanzania wote,"amesema Askofu Ouma.
Pia, amewaomba Wakristo na Watanzania kwa ujumla, kudumu Katika kutenda matendo mema na kujiepusha na dhambi. Huku akisema ufufuko wa Yesu Kristo umeleta ukombozi ulimwenguni hivyo kila mmoja aenende katika matendo mema na kumcha Mungu kwa unyoofu wa moyo.
Aidha, Askofu Ouma amewasisitiza wazazi na wezi kusimamia malezi bora na maadili mema ya watoto wao katika kuwaandaa kuwa tegemeo kwa siku za usoni kuleta manufaa katika jamii na taifa kwa ujumla.
Katika ibada hiyo, Askofu Ouma ameongoza maombi maalumu ya kumuombea Rais Mheshimwa Samia Suluhu Hassan, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya, Wabunge, Madiwani, wakuu wa taasisi mbalimbali,Watanzania wote na ustawi wa nchi.