NA DIRAMAKINI
BENKI pekee inayoongozwa na misingi ya Kiislamu kikamilifu Tanzania inayofahamikwa kwa jina la Amana Bank inakaribisha makampuni yote yaliyokamilisha taratibu za kutoa huduma ya bima Takaful Tanzania kuimarisha huduma hiyo kwa kuihusisha na benki inayoendeshwa kwa misingi ya kiislamu.
Akizungumzia juu ya muongozo wa Bima ya Takaful uliotolewa na Mamlaka ya usimamizi wa bima (TIRA) hapa nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank Abubakar Athman (pichani juu), alisema “Kwakuwa misingi ya dini ya kiislamu hairuhusu kufanya biashara na bima za kawaida ilikuwa ni changamoto sana kwa Benki yetu.
"Tulikuwa tunatumia mlango wa dharura kufanya miamala na Bima za kawaida. Sasa, mambo yanaelekea pahala pazuri na tunaishukuru sana serikali kupitia TIRA kwa kuwezesha upatakanaji wa huduma hii muhimu ya fedha, Jambo ambalo litatuwezesha kufanya miamala na wateja wetu kwa kutumia bima zinazofata utaratibu unaokubalika katika misingi ya Kiislamu katika kujikinga na majanga mbalimbali, ijulikanayo kama Takaful".
Aliendelea kusema "Huduma za bima za Takaful zinaimarisha zaidi mfumo wa fedha unaofata misingi ya kiislam katika soko na umejengwa katika misingi ya kusaidiana katika majanga bila kudhulumiana".
Amana Bank imezitaka kampuni zinazolenga kutoa huduma ya Takaful kuzingatia maadili ya uwekezaji wa fedha zitokanazo na uwekezaji au wachangiaji wa mfuko kwenda sambamba na muongozo ulitolewa na TIRA
Aidha, katika kuimarisha huduma hii, Amana Bank itatoa ushauri wa bure kabisa kwa wateja wake kupitia kitengo chake cha Bidhaa na Sharia. Amana Bank imejiimarisha katika kuhakikisha Kutoa mchango wa kuendeleza na kukuza sekta hii tanzu ili huduma zake ziweze kupatikana na kuwafikia wateja wake na wananchi kwa ujumla.
Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dk. Baghayo Saqware, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kanuni na miongozo ya kutoa huduma za Bima kupitia Benki.
Mfumo wa fedha unaofuata misingi ya kiislamu (Fiq Muamalat and Islamic Finance Jurisprudence) inahitaji kuwepo na mihimili mikuu mitatu ambayo ni Islamic Banking, Islamic Insurance pamoja na Islamic money markets & capital markets (Masoko ya fedha na mitaji).
Kuanzishwa kwa Takaful sio tu unaongeza wigo wa huduma za bima nchini, bali unaziwezesha Bank zinazofuata misingi ya sharia kikamilifu kukidhi vigezo vya vinavyohitajika katika utoaji wa huduma zake kikamilifu na kuwapatia wananchi huduma za bima katika misingi ya udugu,umoja, haki na uadilifu.