NA DIRAMAKINI
MKURUGENZI wa Mtandao wa Kijamii wa U turn Collection, Allen Mhina (31) na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashtaka matatu yakiwemo ya kuchapisha maudhui yanayokiuka haki na uhuru wa mtu mwingine na kumfedhesha mtu kwa njia ya mtandao.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 57/2022 ni Mtandao wa U turn Collection na Mange Kimambi App.
Mhina na wenzake wamesomewa mashtaka yao, Ijumaa ya wiki iliyopita mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na mawakili wa Serikali Waandamizi, Slyvia Mitanto akishirikiana na Mwanaamina Kombakono.
Wakiwasomea hati ya mashtaka, katika shtaka la kwanza, ambalo ni kuchapisha maudhui yanayokiuka haki na uhuru wa mtu mwingine, linalowakabili washtakiwa wote, wakili Mitanto na Kombakono wamedai kuwa, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Machi 9, 2022 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Siku hiyo ya tukio, washtakiwa wanadaiwa walichapisha video ya aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Kitengo cha wagonjwa Mahututi (ICU) maudhui ambayo yanadhuru haki ya faragha ya mgonjwa.
Aidha, shitaka la pili, ni kufanya kazi ya uandishi wa habari bila ya kuwa na kibali kutoka bodi ya ithibati ya wanahabari, shitaka linalomkabili Mhina na U turn Collection.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Septemba 22, 2021 na Machi 14, 2022 Kinondoni eneo la Manyanya, ambapo siku hizo washtakiwa hao wanadaiwa walifanya kazi ya uandishi wa habari bila ya kuwa na kibali kutoka bodi ya ithibati ya wanahabari.
Shtaka la tatu ni kumfedhesha mtu kwa njia ya mtandao (cyber bullying), shtaka linalomkabili Mhina peke yake, analodaiwa kulitenda Machi 9, 2022 katika maeneo tofauti ndani ya nje ya nchi ya Tanzania.
Mshtakiwa Allen kupitia mfumo wa kompyuta unaojulikana kama Mange Kimambi APP unaosimamiwa na U turn Colection anadaiwa kuchapisha video ya aliyekuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kwa nia ya kusababisha dhiki ya kihisia.
Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake, alikana kutenda makosa hayo. Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali( PH) mshtakiwa.
Hakimu Kabate alitoa masharti ya dhamana ambayo mshtakiwa huyo alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh100,000.
Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi April 27, 2022 itakapoitwa kwa ajili ya PH.Hata hivyo mshtakiwa yupo nje kwa dhamana. (Mwananchi)