Bunge la Tanzania kuwa LIVE, fahamu sababu zilizochangia matangazo kusitishwa

*Mwaka 2016 utafiti wa Twaweza ulionesha namna wananchi walivyokuwa na kiu ya kulitazama Bunge mubashara

NA GODFREY NNKO

KATIBU wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi.Nenelwa Mwihambi amesema baada ya maboresho ya Studio ya Bunge na Kamati ya Uongozi ya Bunge kuridhia vikao vya Bunge vitaanza kurushwa mubashara (live) kuanzia kesho Aprili 5, 2022 wakati Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti utakapoanza.
Bi.Mwihambi ameyasema hayo leo Aprili 4, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusiana na hatua hiyo.

Hayo yanajiri ikiwa Januari, 2016, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo alieleza kuwa,hatua ya Serikali kusitisha matangazo hayo kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ilichangiwa na gharama kubwa ambayo ilikuwa inafikia shilingi Bilioni 4.2.

Pia ilionekana asilimia kubwa ya watumishi wa umma walikuwa wanatumia muda mwingi kushabikia mambo yanayoendelea bungeni badala ya kuendelea na kazi ofisini, hivyo kudhoofisha huduma kwa wananchi.

Ndani ya mwaka huo huo, Taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo ya utafiti wake, ambapo ilibainika kuwa asilimia 79 ya Watanzania wamepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Katika maoni yao, wananchi hao walidai kuwa ni haki yao ya msingi kufahamu kinachoendelea katika vikao mbalimbali vya Bunge.

Utafiti wa taasisi hiyo ulifanywa katika maeneo tofauti ya Tanzania Bara kupitia mpango wake wa Sauti za Wananchi.

Akitoa taarifa ya matokeo ya utafiti huo mwaka huo jijini Dar e Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema, suala hilo lilionekana kutokuungwa mkono na wananchi wengi.

“Asilimia kubwa ya Watanzania wanapinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Suala hili limeonekana kugusa hisia za watu wengi na maamuzi haya ya Serikali yakionekana kutoungwa mkono.

“Katika utafiti huu wananchi nane kati ya 10 wanapinga uamuzi wa hali inayodhihirisha kutoungwa mkono kwa hatua hiyo,” alisema Eiyakuze mwaka 2016 wakati akiwasilisha taarifa ya utafiti huo.

Akizungumzia sababu walizozitoa wananchi wanaotaka matangazo ya Bunge yarushwe moja kwa moja, Eiyakuze alisema asilimia 46 walisema yanawafanya waweze kufuatilia utendaji wa wabunge waliowachagua kwa kuwa huko ndio walikowatuma.

“Asilimia 44 wanasema ni muhimu kwa sababu wananchi wanahaki ya kufahamu kinachoendelea bungeni, asilimia 29 wanasema matangazo ya moja kwa moja yalikuwa yanaaminika zaidi kwa watazamaji na wasikilizaji kuona na kusikia wenyewe kile kinachoendelea tofauti na mfumo wa kurekodi ambapo kuna baadhi ya mambo yanahaririwa.

“Asilimia 16 walidai kuwa ina fursa mwananchi kupata taarifa sahihi badala ya kuzisoma kwenye magazeti huku asilimia 16 nyingine wakisema inawasaidia wananchi kufuatilia mijadala ya Bunge kwa wakati,”alisema Eiyakuze.

Pamoja na hali hiyo mkurugenzi huyo alisema katika utafiti huo asilimia 92 ya wananchi walisema kuna umuhimu wa vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja kupitia runinga na redio bila kujali gharama zilizoelezwa kuwa ndio chanzo cha kufikia uamuzi huo.

“Asilimia 88 walisema vipindi vya Bunge virushwe ‘Live’ bila kujali gharama ukilinganisha na asilimia 12 ambao waliona ni muhimu suala la bajeti likazingatiwa,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema asilimia 80 wanaona matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni ni muhimu kama yalivyo na asilimia 20 wakisema fedha hizo zitumike kwenye huduma nyinge za jamii.

Pia utafiti huo ulionesha Watanzinia wanne kati ya kumi wamewahi kuangalia matangazo ya moja kwa moja kupitia runinga na sita kati ya kumi wamesikiliza kupitia redio.

Aidha utafiti huo umeonyesha zaidi ya nusu ya wananchi waliosema wameangalia au kusikiliza vipindi vya Bunge walifanya hivyo ndani ya miezi miwili iliyopita katika mwaka huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news