COSTECH yawaongezea wahariri maarifa ya kisayansi na kiteknolojia

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imewakutanisha pamoja wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari kwa lengo la kuwaongezea maarifa katika eneo la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STU).
Sehemu ya wahariri wakiendelea kujadiliana wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na CHOSTECH kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya ushirikiano ili umma wa watanzania upate habari zinazohusu sayansi,teknolojia na ubunifu.

Lengo ni kuhakikisha jamii ya watanzania inaendelea kupata habari zilizochakatwa kwa viwango bora za sayansi, teknolojia na ubunifu kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Aidha,kupitia mafunzo hayo wahariri wamehaidi kuendelea kusambaza habari za sayansi na teknolojia kwa ufanisi.

Wametoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa warsha ya mafunzo ya kutazamia nafasi ya wahariri katika uzalishaji na usambazaji wa habari za sayansi, teknolojia na ubunifu iliyoandaliwa na COSTECH kupitia Kurugenzi ya Menejimenti ya Maarifa (DKM) COSTECH ili kutengeneza mkakati madhubuti utakaosaidia kuzalisha na kusambaza makala nyingi zaidi za mafanikio ya miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ili wananchi wafahamu kazi kubwa inayofanywa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Bugwesa Katale akifungua mafunzo hayo amesema kwamba, COSTECH ni taasisi ya umma na moja ya jukumu lake kubwa ni kuishauri Serikali pamoja na kuratibu na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu hapa nchini, kwa kuandaa ajenda za utafiti za Utafiti na uandaaji wa nyaraka mbalimbali za namna ya kuongoza tafiti na bunifu zinaweza kuendeshwa hapa nchini.

“Leo tuko hapa katika kuhakikisha tunaendeleza jukumu la kusambaza habari za sayansi, teknolojia na ubunifu na ubinifu. Vilevile tume ina kurugenzi nne ambazo ni Usimamizi na Kurugenzi ya Uendelezaji wa Tafiti, Kurugenzi ya Menejimenti ya Maarifa, Kurugenzi ya Huduma za Taasisi na Kurugenzi ya Uhawalishaji wa Teknolojia na zinafanya kazi pamoja ili kuhakikisha tunapata matokeo,”amesema.

Dkt.Bugwesa ameongeza pia tume ina vitengo vinavyosaidia utekelezaji wa kazi zake na mojawapo ni Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) kazi yake kubwa ni kufadhili miradi ya utafiti na ubunifu nchini.
Awali Kaimu Mhariri wa Gazeti la Habarileo Mgaya Kingoba, ameipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wahariri kwani yamewajengea uwezo mkubwa kuelewa na kuongeza COSTECH ni wadau muhimu na wanamchango mkubwa kuhakikisha habari zinatoka.

Amewashauri COSTECH waendelee kuwashirikisha waandishi wa habari na wahariri ili waweze kutoa taarifa katika lugha rahisi na wananchi waweze kuelewa dhana nzima ya matumizi ya tafiti.

Kwa upande wake, Shamuna Said ambaye ni Mhariri wa Habari kutoka kitengo cha Habari na Matukio TBC aliwapongeza COSTECH na kuongeza kuwa mafunzo hayo yana manufaa zaidi ambapo yataenda kutoa habari kwa lugha rahisi na kutatua changamoto ya bunifu na matokeo ya tafiti kubaki kwenye makabati bila kuwafikia walaji wa mwisho ambao ni wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt.Bugwesa Katale (wa kwanza kulia waliokaa),maofisa wa tume hiyo pamoja na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika picha ya pamoja.

“Haya mafunzo ni muhimu kwa sisi wahariri tunaozalisha vipindi na habari mbalimbali ili bunifu na tafiti ziweze kuwafikia walengwa ambao ni wananchi,”amesema.

Kabla ya kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa kutoka COSTECH, Dkt. Philibert Luhunga aliwashukuru wahariri kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kusisitiza kuja na mkakati shirikishi utakaosaidia kuendeleza ushirikiano baina yao ili kufikia matamanio ya kuendesha Taifa kwa sayansi na teknolojia na hatimae kufikia maendeleo kwa ufanisi mkubwa ili jamii ya Kitanzania inufaike kwa tafiti pamoja na bunifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news