NA DIRAMAKINI
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Mgoma ameshuhudia namna Kadi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inavyomsaidia yeye na familia yake katika kupata huduma za matibabu.
Amesema bila kuwa na Kadi hiyo angekuwa na mzigo mkubwa sana katika eneo la matibabu hivyo amewaomba wananchi kutofanya mchezo katika kuamua kujiunga na NHIF.
Hayo ameyasema leo wakati alipotembelea banda la NHIF katika viwanja vya CCM Jijini Dodoma kwenye Maonesho ya Wiki ya Usalama Mahali pa Kazi ambapo Mfuko unatoa huduma mbalimbali ikiwemo ya elimu na uandikishaji wa wanachama.
Ameongeza kuwa, kadi ya NHIF imekuwa na heshima kubwa katika vituo vyote vya kutolea huduma na kwa sasa imeondoa mitazamo hasi ya kunyanyapaliwa kwa wanachama wa Mfuko.
“Nawasihi sana wananchi wasifanye mchezo na eneo la kujiunga na NHIF kwa sababu maisha ya sasa bila kuwa na bima ya afya ni ngumu sana kumudu gharama za matibabu,” alisisitiza.