NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar limesema msichana aliyetoa tuhuma mitandaoni,Bi.Zainab Oladehinde (23) kuwa amedhalilishwa akiwa Zanzibar ni kulihujumu jeshi hilo na utalii wa visiwa hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 18, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Martin Otieno alisema msichana huyo, Zainab Oladehinde (23), raia wa Nigeria ametoa tuhuma za kudhalilishwa akiwa katika hoteli moja eneo la Nungwi mkoani humo.
Alisema Aprili 18, mwaka jana majira ya saa 4:00 usiku polisi katika Kituo cha Polisi Nungwi walipokea taarifa kutoka kwa Zainab akiwa hotelini hapo kuwa watuhumiwa Ezekiel Joseph na Mohamed Juma walifika kwa nyakati fotauti katika chumba chake kwa nia ya kutenda kosa.
Alisema, mlalamikaji alidai kuwa watuhumiwa hao walimshika na kumchezea maeneo ya kifuani na kumshika mwili wake pamoja na kumuibia dola za Marekani 1,100. “Baada ya kupokea malalamiko hayo Jeshi la Polisi lilianza kufanya uchunguzi kwake.
"Hata hivyo, baada ya mlalamikaji kufika kituoni alikuwa akimshinikiza Mkuu wa Kituo kuwa yeye anataka alipwe fedha dola za Marekani 10,000 na uongozi wa hoteli hiyo jambo ambalo jeshi hilo halikustahiki kusimamia katika kituo cha polisi.
"Zainab alieleweshwa hilo, lakini hakuwa tayari kukubali ushauri huo na alielimishwa kuwa kama anataka kulipwa ni vyema afungue madai hayo mahakamani na polisi ibaki na madai yake ya msingi ya kudhalilishwa na kuibiwa,”alisema Kamanda Otieno.