NA SOPHIA FUNDI
WENYEVITI wa mamlaka ya mji mdogo wa Karatu mkoani Arusha wametakiwa kuwahamasisha wananchi kushiriki katika matukio mbalimbali ya kitaifa yanayoendelea ikiwemo zoezi la anwani za makazi pamoja na zoezi la chanjo ya polio inayoendelea kufanyika nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Karatu, Faraja Msigwa wakati akizungumza na wenyeviti hao katika kikao cha Baraza la Mamlaka hiyo.
Msigwa alisema kuwa, mwenyekiti wa kitongoji ni kiungo muhimu katika matukio yanayoendelea hivyo ni jukumu lao kushirikiana na wataalam wanaopita katika maeneo yao kwa ajili ya anwani za makazi ambapo alisema endapo zoezi hilo litakamilika vizuri litarahisisha zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, mwaka huu.
Pia aliwataka wenyeviti hao kusimamia miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika maeneo yao, kwani serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo wilayani Karatu ambapo alisema ni wajibu wa mwenyekiti wa kitongoji kuwahamasisha wananchi kujitokeza kufanya kazi za mikono pale inapotakiwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mamlaka ya mji huo, Yuda Morata aliwaomba wenyeviti kushirikiana na wataalam wanaopita kwenye maeneo yao kwa kuanisha maeneo yatakayowekwa vibao kwa kutoa elimu kwa wadau mbalimbali na wananchi.