NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KIKOSI cha KMC FC leo kimefanya maandalizi yake ya mwisho kuelekea katika mchezo wake wa Ligi kuu ya NBC Soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi utakaopigwa hapo kesho katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam saa 16:00 jioni.

Kutokana na barua hiyo ya TPLB,Afisa Habari na Mahusiano wa KMC FC,Christina Mwagala amesema,Timu ya Manispaa ya Kinondoni inarejea sasa katika uwanja wake wa nyumbani ikiwa ni baada ya kupita kwa takribani michezo mitano ikicheza nje ya uwanja huo na hivyo kulazimika kutumia uwanja wa Azam Complex Chamanzi ambapo mara ya mwisho kutumia uwanja huo wa Uhuru ilikuwa ni kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Azam FC na KMC kupata ushindi wa magoli mawili kwa moja.
Amesema,KMC FC chini ya Kocha Mkuu Thierry Hitimana hadi sasa imejiandaa vema kweye mchezo huo licha ya kuwa na ushindani mkubwa kutokana na kwamba Timu ya Namungo imekuwa ikifanya vizuri katika michezo yake, lakini ubora wa wachezaji pamoja na benchi zima la ufundi litahakikisha kuwa alama tatu muhimu zinapatikana.
“Tumetoka kupoteza michezo miwili mfululizo, na tunakwenda kwenye mchezo mwingine tukiwa nyumbani, hii ni nafasi kwetu ya kusahihisha makosa ya awali na Kocha Mkuu Hitimana katika kipindi hiki ambacho timu zilikuwa kwenye mapumziko kupisha kalenda ya FIFA amefanya maboresho kwenye maeneo ambayo aliona yana changamoto ambazo zilikosesha timu kupata matokeo mazuri, hivyo mashabiki zetu watarajie kupata burudani.

Aidha,Klabu ya KMC FC imewasihi mashabiki kujitokeza kwa wingi siku ya kesho kwenye mchezo huo muhimu ambao wachezaji wamejiandaa vizuri kuhakikisha kwamba wanatoa burudani iliyoambatana na ushindi, ukizingatia kuwa itakuwa siku ya wikiendi.