Kirama:Tume ya Utumishi wa Umma ni chombo rekebu na Mamlaka ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma

NA DIRAMAKINI

KATIBU wa Tume ya Utumishi wa Umma,  Bw. Mathew M. Kirama amesema, tume hii ni chombo rekebu na Mamlaka ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 ya mwaka 2002 (Marejeo ya mwaka 2019).
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama (wa tatu kutoka kulia) katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Tume ya Utumishi wa Umma mara baada ya kufungua mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati jijini Dar es Salaam leo. Wa nne kutoka kulia ni Bibi Martha A. Wililo, Mwenyekiti wa Kamati. (Picha na PSC).

Bw. Kirama amesema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi ya Tume ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Ukumbi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Jijini Dar es Salaam.

"Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 Kifungu cha (10) kimeainisha majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma kuwa ni pamoja na Ushauri na Urekebu. Tume ni chombo rekebu chenye Mamlaka na Wajibu wa kuhakikisha kuwa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma yanasimamiwa na kuendeshwa kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu mbalimbali kama inavyotolewa na Mamlaka," amesema Bw. Mathew M. Kirama.

Akifafanua zaidi amesema, ili kuhakikisha malengo ya kuimarisha Utawala Bora katika Utumishi wa Umma yanafikiwa. Tume hupokea na kutolea uamuzi rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma na kufanya ukaguzi wa uzingatiaji wa masuala ya Rasilimali Watu kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma. 

Tume, huwajengea uwezo wadau wake ili waweze kutafsiri na kutekeleza ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

Bw. Mathew M. Kirama amesema kuwa, lengo la mafunzo haya kwa Kamati ya Ukaguzi ya Tume ni kuinua kiwango cha ujuzi na uelewa kwa Kamati na ni utekelezaji wa Kifungu cha 3 (12) cha Mwongozo wa Kamati ya Ukaguzi Toleo la Pili la mwaka 2019. Vile vile, kujifunza na kuinua uwezo wetu wa utendaji katika Kamati ya Ukaguzi ya Tume ya Utumishi wa Umma.

“Kupitia mafunzo haya nina imani mtapanua uelewa wenu kuhusu Tume, ninafahamu kazi ya Kamati hii ni kumshauri Afisa Masuuri, katika utendaji wake wa kila siku. Hivyo, ni muhimu sana kwenu kuifahamu Tume ambayo ndiyo Taasisi ninayoiongoza ili jukumu lenu la “oversite” mlifanye vema kabisa. Bila kufahamu vizuri majukumu ya Tume haitakuwa rahisi sana kutekeleza kazi yenu ya kushauri,"amesema Bw. Kirama.

Katibu wa Tume, Bw. Mathew M. Kirama amehitimisha kwa kutoa wito kwa Kamati kuendelea kufanya kazi kwa Bidii na Juhudi kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais kuleta maendeleo. 

"Kamati kama hizi zinazotusimamia zikifanya vizuri zitatoa mchango mkubwa kwa Tume na kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania,"amesema.

Kwa upande wake Bw. Bernard Marcelline, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu akiwasilisha mada kuhusu tume na majukumu yake alisema Utumishi wa Umma upo kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi. Watumishi wa Umma wapo kwa ajili ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, hivyo ni lazima wasimamiwe vizuri kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyotolewa.

"Ni muhimu kuwa na chombo cha kutekeleza jukumu la Urekebu, chombo chenyewe ni Tume ya Utumishi wa Umma,"amesema Bw. Marcelline.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news