*Wanafunzi 1,500 wafundishwa na walimu wawili waliopo kwa sasa
NA MOHAMED HAMAD
KUTOKANA na uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi, wanafunzi zaidi ya 1,500 wa Shule ya Sekondari Kiteto iliyopo mkoani Manyara wanafundishwa na walimu wawili waliopo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiteto, John Kimaro akizungungumza mbele ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kiteto kwenye mahafali ya kidato cha sita amesema,idadi ya wanafunzi Kiteto Sekondari haiendani na ikama ya walimu waliopo.
"Mheshimiwa Mwenyekiti hapa tuna walimu 37 tu, na tuna zaidi ya wanafunzi 1,000 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita tunachangamoto kubwa ya ufundishaji kwa uwezo wako tunaomba msaada wa kupatiwa walimu.
"Kwa kuwa wewe unayo nafasi ya kuonana na viongozi mbalimbali tufikishie kilio chetu huko,tunaomba utuondolee hii adha, kwani hawa wanafunzi wanaendelea kukosa masomo.Haki ya elimu kwa mwanafunzi iko kikatiba, kwani huwezi amini hapa tuna walimu wawili tu wa masomo ya Sayansi, tunapaswa kuwa na zaidi ya hao ili tutoe huduma, lakini unawezaje kuingia madarasa yote walimu wawili?,"amesema.
Akizungumzia uhaba wa walimu, Mhe Abdalah Bundala, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mbele ya wanafunzi na walimu na wazazi aliwaahidi kuwa atashughulikia tatizo hilo, kwani mpaka sasa pamoja na uhaba wa walimu hao shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri.
Nao baadhi ya wanafunzi akiwemo James Elieta kidato cha sita amesema, pamoja na uhaba wa waalimu unachochea utoro kushuka kiwango cha elimu pamoja na wanafunzi kutofikia ndoto zao kikamilifu zipo jitihada kubwa ambapo mwaka jana walipata ufaulu wa division 1 poiti saba.
Amesema awali wazazi walilazimika kutumia gharama kubwa kuwatafutia watoto wao shule nje ya wilaya na maeneo mengine ya Kiteto hivyo kupatikana shule hiyo kumepunguza gharama kwa wazazi pamoja na kuongeza idadi ya wasomi nchini.