NA FRESHA KINASA
MKUU wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, Dkt. Halfan Haule amezindua Kituo cha Kukuza ubunifu kilichofadhiliwa na Bismart Brands Academy chini ya Mkurugenzi wake Boniphace Ndengo ambapo amewataka Wananchi wa makundi yote kukitumia kituo hicho kukuza ubunifu wao, ujuzi na kutangaza fursa zao ikiwemo ujasiriamali katika kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Dkt. Haule ameyasema hayo leo Aprili 21, 2022 kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Justine Manko wakati wa uzinduzi wa kituo hicho ulioendana sambamba na Uzinduzi wa Kampeni ya "Tumia Maktaba, Ongeza Maarifa Kukuza Ubunifu".

Manko amesema, iwapo kituo hicho kitatumiwa kikamilifu kitachangia kwa kiwango kikubwa kuleta mapinduzi chanya hususan kuwaongezea maarifa yatakayosaidia kukuza ubunifu wao na ujuzi pia na kuleta tija katika maisha yao na taifa.
Aidha, amempongeza Mkurunzi wa Bismart Brands Academy, Boniphace Ndengo kwa juhudi na ubunifu ambao amekuwa akiufanya kuchangia kusukuma mbele maendeleo ya Mkoa wa Mara, jambo ambalo amesema linapaswa kuungwa mkono.
Pia amesisitiza teknolojia katika huduma za maktaba katika utoaji wa maarifa kwa wananchi ni muhimu kuwezesha kuwafikia wananchi wengi zaidi huku akiwahimiza wanafunzi wa vyuo, shule za sekondari na wananchi wote kuitumia maktaba ya Mkoa wa Mara kujifunza mambo mbalimbali ya muhimu.

Amesema, Bismart Brands Academy inaamini kwamba, ubunifu, sayansi na ujasiriamali ndio nguvu tatu kubwa zilizotumika kujenga uchumi wa mataifa makubwa duniani, mabilionea wakubwa, makampuni yanayotikisa dunia na kwamba vitu hivyo vitatu havijatiliwa maanani zaidi hapa nchini na Afrika kama inavyotarajiwa.
"Utafiti wetu mdogo unaonesha muunganiko wa vitu hivi vitatu ubunifu, ujasiriamali, na sayansi ndio uliozaa teknolojia zote tunazoziona leo biashara na pia maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanayoshuhudiwa duniani. Muungano wa nguvu hizi ndio umezaa nguvu ya mataifa makubwa duniani,"amesema.

Amesema, mjasiriamali ni mtu mwenye nguvu kubwa ya ubunifu, uthubutu, maono na mwenye uwezo wa kuunganisha fursa na rasilimali ili kuanzisha miradi mikubwa na midogo inayolenga kutatua changamoto zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla.

"Leo ukiuliza mwanasayansi ni nani, watu wengi watakwambia ni mtu aliyesoma masomo ya Fizikia, Kemia, na Biolojia na kumbe Mwanasayansi ni Mmu mwenye uwezo wa kudadisi, kugundua na kuunda kanuni zinazozalisha matokeo yanayotarajiwa na yenye manufaa. Bismart Brands Academy tumejipa wajibu wa kuwa mabalozi wa kusaidia kuelimisha, kuhamasisha, kuchochea na kuwezesha matumizi sahihi ya nguvu sahihi ya ubunifu, sayansi kwa nchi za Afrika tukianza na Tanzania,"amesema Ndengo.
Ameongeza kuwa, Bismart Brands Accademy inaendelea kushirikiana na Bodi ya Huduma za Maktaba na chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na kilimo kuzindua kampeni hiyo ya TUMIA MAKTABA, ONGEZA MAARIFA KUZA UBUNIFU kampeni itakayodumu kwa miaka mitatu.
Ambapo kwa sasa baada ya kuzinduliwa katika Mkoa wa Mara kampeni hiyo itaenezwa sehemu mbalimbali ikiwemo shuleni na vyuoni. Ambapo kampeni hiyo imezichagua maktaba zote nchini kwa kuanza na Mkoa wa Mara kuwa vituo vya kukuza ubunifu.

Kampeni hiyo na mpango huo unatarajiwa kuzalisha fursa za ajira mpya milioni moja katika kipindi cha miaka mitatu.
Mkutubi wa maktaba ya Mkoa wa Mara, Sakina Msuya amesema kuwa, maktaba hiyo inatoa huduma mbalimbali na inawachama wapatao 4,324. na inatoa huduma za mtandao, machapisho, majarida, vitabu, magazeti na akasema iwapo mbunifu ana jambo lake, anauwezo wa kupata maarifa yake maktaba kujifunza.